|
Bravo JK: Mifarakano ya kidini ni hatari hakika
2006-10-26 09:24:43
Na Mhariri
Katika hotuba yake kwenye Baraza la Idd el Fitr, Rais Jakaya Kikwete alitoa onyo kali kwa watu wenye mwelekeo wa kupandikiza chuki za kidini hapa nchini.
Katika hotuba hiyo aliyotoa mjini Arusha ambako Baraza la Idd lilifanyika, Rais Kikwete alisema hakuna sababu yoyote ya waumini wa dini mbalimbali kugombana, kwa sababu hakuna atakayeibuka mshindi katika ugomvi huo.
Alifafanua kwamba dini na madhehebu mbalimbali yataendelea kuwepo daima na hivyo ni bora watu wakajenga utamaduni wa kuvumiliana kiimani.
Alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kulinda amani na umoja wetu bila woga wala upendeleo kwa dini yoyote.
Bila shaka, Rais alitoa karipio hilo kufuatia kuibuka kwa makundi ya kidini ambayo yamekuwa yakitoa mahubiri yanayoonekana kukashifu dini zingine.
Mahubiri hayo katika baadhi ya maeneo hapa nchini yaliwahi kusababisha mitafaruku mbalimbali iliyotishia amani.
Wakati fulani katika miaka ya karibuni hali ilikuwa mbaya zaidi kiasi cha kusababisha waumini kufikishana kortini kwa madai ya kukashfiwa na waumini wa dini zingine kwenye mihadhara.
Ilifikia wakati watu walianza kuogopa kuhudhuria mihadhara hiyo kwa hofu ya kutokea ghasia kutokana na lugha kali na za uchochezi zilizokuwa zinatumika katika mihadhara hiyo.
Tunaelewa kwamba mihadhara ni mojawapo ya njia zinazotumika kufikisha ujumbe wa kiroho kwa waumini wa dini husika, lakini mihadhara hiyo inapotumika kupandikiza chuki za kidini, hapo tutakuwa tunaitumbukiza nchi yetu kwenye kisima cha machafuko.
Na machafuko hayo yatakaposhika kasi, ni dhahiri waathirika watakuwa waumini wa dini zote hasa kwa kuzingatia kuwa vita inapotokea haibagui asilani.
Kama alivyosema Rais Kikwete, nchi yetu imefanikiwa kwa miaka mingi kulinda amani na umoja wetu, sasa iweje leo tuharibu amali hizo kwa sababu ya wakorofi wachache wasioitakia mema nchi yetu?
Nchi yetu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuzika ukabila.
Tumeuzika ukabila kwenye kaburi lenye kina kirefu sana, ambalo anayediriki kulifukua hawezi kufika mwisho kabla naye hajazikwa.
Kwa hili la ukabila, nchi yetu ni mfano wa kuigwa popote. Ni muhimu pia tukatae fukuto za udini ili kulinda umoja wetu wa kitaifa ambao hakika tumeujenga kwa miaka mingi sana.
Kwa msingi huo, ni muhimu kwa waumini kuthamini imani zao na wakati huo huo kuheshimu imani za wengine ikiwa ni nguzo na njia pekee ya kudumisha umoja wetu wa kitaifa.
|