|
Nani alisema ana moto na shirikisho la afrika mashariki?
2006-10-26 09:26:46
Na Maakwaia wa Kuhenga
Sijasikia, na shidhani na wewe msomaji wa safu hii umesikia wananchi wa kawaida popote pale wakililia Shirikisho hata kwa nyimbo katika maholi ya muziki kinyume na miaka ya sitini baada ya Uhuru wa nchi za Afrika Mashariki ambako kulikuwepo nyimbo za kutaka Shirikisho.
Sasa moto wote huu umetoka wapi? Ni dhahiri umetoka kwa viongozi wetu. Wakishapiga suti zao na kupongezana huko Arusha na Nairobi kwa brandy na whisky na kuongea kwa kimombo kizuri, na wao wenyewe kujipigia mahesabu watachukua nafasi gani katika hiyo serikali ya Shirikisho ndipo wanakuja na mpya kama walivyo na moto hivi sasa!
Viongozi walio karibu na wananchi wao mpaka sasa wangekuwa wameshafahamu hisia au mood za wananchi wao.
Wangekuwa wameshafahamu kuwa kipa umbele cha wananchi hivi sasa ni kupatikana kwa ajira na kukidhi haja zao za kila siku.
Wangekuwa wameshafahamu mpaka sasa kuwa hata katika hali ya sasa ambapo ipo Jumuia la kiuchumi la Afrika Mashariki (EAC) tayari kuna malalamiko ya kinyanganyiro katika soko la ajira.
Hivi sasa Watanzania wanalalamika kuwa ajira ambazo zingekuwa halali kwa wananchi wa nchi hii sasa zimo mikononi mwa Wakenya na Waganda ambao wapo hapa nchini kwa wingi hivi sasa.
Watu walisema takrima huanzia nyumbani au charity starts at home. Kulikoni badala ya kuanza kula wewe na watoto wako nyumbani kwako mkala mkashiba, haya mambo ya kuanza kuita majirani waje kula chakula nyumbani kwako ambacho kwanza hakitoshi yanaanzia wapi?
Nimegusia hapo mwanzo jinsi moto wa kutaka Shirikisho ulipoanzia kutoka chini kwa wananchi mpaka wakaanza kuimba nyimbo wakitaka Shirikisho.
Sababu za wananchi kutaka shirikisho zilikuwepo wakati huo kwa kuwa walijua tutaondokea wote pamoja kama mataifa matatu machanga, tutavuta upande mmoja na siyo kila mtu kivyake.
Sababu za wananchi za miaka hiyo ya sitini sasa hazipo. Kenya ilijenga ubepari kwa maana ya wachache kuwa matajiri na wengi kutopea katika ufukara.
Tanzania ilijenga ujamaa kwa maana ya kugawa rasili mali za taifa kwa masilahi ya wengi na kwa kiwango kikubwa ilifanikiwa katika hili kwa kuwa hakukuwa na tatizo kubwa la ajira kama ilivyo hivi leo na viwanda vilikuwepo.
Uganda haikuwa tofauti sana na Kenya katika hili ingawa yenyewe, kinyume na nchi nyingine katika Afrika Mashariki ilionja joto la jiwe la udikteta wa utawala wa kijeshi na baadaye vita vya wenyewe ambavyo ndiyo sasa tu vinaanza kufifia.
Kama kuna kitu kinachounganisha nchi hizi tatu ni mfumo wa uchumi wa GULIO au ubepari. Katika nchi hizi tatu, Tanzania ni limbukeni katika mfumo huu, Kenya ni kungwi mzoefu na mwerevu wa maisha ya mwituni wa mnyama mkubwa kumla mdogo na Uganda ni mwerevu wa uchumi wa gulio kwa mahesabu ya kisomi. Hapo nimesema kikubwa; ni matumaini yangu umenifahamu!
Kuna kitu kingine pia kinachounganisha nchi hizi tatu. Nacho ni kwamba nchi hizi zote zimo katika mfumo wa uchumi wa gulio, hakuna hata nchi moja inayoweza kujidai kuwa haina tatizo la ukosefu wa ajira kwa mfano.
Katika nchi hizi tatu, watu wengi wanazidi kuwa masikini, na wachache, hasa viongozi wanazidi kuwa matajiri.
Tunapoongelea uchumi wa gulio kwa upana wake maana yake ni kuwa wakala wa mataifa makubwa kiuchumi na mashirika makubwa ya biashara duniani, yaani multinationals.
Kamwe nchi za uchumi mkubwa duniani hazitapendelea na zitahakikisha kuwa nchi kama hizi zetu zinabaki soko tu la bidhaa kutoka nchi hizo na kuhakikisha hakujengwi viwanda katika nchi hizi ambazo zitaleta changamoto kwa uhodhi wa bidhaa kutoka ngambo.
Ushahidi wa hili ni kuzagaa kwa bidhaa kadha wa kadha ambazo zote ni za nje kutoka Dar es Salaam mpaka Kampala.
Ndani ya Tanzania, kwa mfano, tunaona kufurika kwa kila aina ya bidhaa na hakuna hata bidhaa moja inayotengenezwa nchini hapa.
Maana rahisi ya hali hii ni kwamba nchi haina viwanda na kama vipo ni vya kuhesabu kwa vidole vya mkono, na kwa maana hiyo hamna ajira.
Sasa katika hali kama hii, ambapo matatizo ni makubwa katika nchi hizo zote tatu, unapoleta Shirikisho, kwa maana ya serikali ya Shirikisho maana yake nini? Unaongeza au unapunguza matatizo?
Wewe kama ni mtu wa nadharia utasema kwamba tukiwa na Shirikisho maana yake ni kuwa na nguvu kubwa zaidi kiuchumi, kuwa na soko kubwa zaidi kwa bidhaa zetu na pia tutakuwa soko kubwa zaidi kimataifa kama watu wamoja wa Afrika Mashariki na maana yake pia kuongelea idadi ya watu zaidi ya milioni 90 wa Afrika Mashariki.
Hoja hii ni sawa. Lakini inabaki nadharia tu kama ilivyo nadharia. Kwa sababu viwanda vyenyewe vya Afrika Mashariki viko wapi?
Tutakachofaulu kufanya tukiunda Shirikisho haraka haraka, maana yake tutafaulu katika kuyazuungusha matatizo yetu kutoka nchi hadi nchi kuja kunyanganyiana chakula ambacho hakipo, na kama kipo hakitoshi kushibisha matumbo zaidi ya majirani!
Wale majirani zetu niliowazungumza hapo nyuma kama ni makungwi wazoefu wa maisha ya mwituni watajazana Tanzania, na kwa sababu watu wetu walio wengi hawajui utajiri wa ardhi wao wanaona ni mapori tu, watajikuta wapangaji katika ardhi yao wenyewe!
Tayari kuna malalamiko kuwa baadhi ya jamaa kutoka nchi jirani wameanza kuchukua na kuhodhi ajira ambazo kwa kawaida zingekuwa za Watanzania na ukichunguza sana sababu kubwa ya kupendelewa wao kupata ajira ni kujua Kimombo zaidi!
Sasa tunayo Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) ambayo kimsingi ni jumuia ya uchumi baada ya kufufua jumuia ile ya kwanza iliyokufa mwaka 1977.
Hivi tumeshajifunza ni kitu gani kilisababisha jumuia hiyo ya zamani kufa? Ni kitu gani hicho ambacho kinatupa uhakika kuwa hii ya sasa haitakufa kwa sababu hizo hizo za kwanza?
Hizi taasisi na demokrasia na utawala tulizonazo katika nchi hizi tatu zimekomaa kiasi gani? Kwa mfano, kama Rais Museveni ameweza kukunja katiba ya nchi yake na kuendelea kutawala muhula wa tatu, sifa hii ya kukunja Katiba ya nchi yake inampa uhalali gani wa kuwania Urais wa Shirikisho la Afrika Mashariki?
Kwa nini tusiimarishe kwanza Jumuia hii ya uchumi (EAC) tuliyonayo sasa na kukomaza taasisi za demokrasia na utawala ndani ya nchi zetu kwanza kabla ya kurukia Shirikisho?
Makwaia wa KUHENGA ni Mwandishi Mwandamizi. E-mail: utafiti@yahoo.com
|