27 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nafasi ya wasomi katika Bunge la Afrika Mashariki
 
2006-10-27 08:45:35
Na LUDGER KASUMUNI

Wasomi wengi wamejikita kugombea nafasi ya Ubunge wa Afrika Mashariki safari hii wakiwa na sababu mbalimbali hususani kuchangia katika mijadala ya kuboresha jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na kuzingatia maslahi ya Watanzania.

Miongoni mwa wasomi waliojitosa kugombea ubunge wa Afrika Mashariki ni Dk. Michael Ndanshau, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa mujibu wa Ndanshau ameamua kugombea nafasi hiyo kwa nia ya kuona kama anao uwezo wa kutumikia umma.

Kimsingi anasema ushiriki wake katika Bunge la Afrika Mashariki ni sehemu ya ajira kwa kuwa wanahitaji watu wenye uwezo wa kufuatilia masuala ya bunge hilo kwa umakini mkubwa.

”Mambo mengi katika bunge la Afrika Mashariki nayaona ni ya kiuchumi hivyo nikishiriki naweza kutoa mchango wangu kwa ukaribu, kama mchumi,” anasema Ndanshau.

Anasema mmoja ya agenda katika bunge hilo ni kuanzisha sarafu moja, hivyo hilo ni eneo zito ambalo anao uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuhusu uanzishwaji wake.

”Uanzishwaji wa sarafu hiyo ni suala la kiuchumi hivyo linahitaji uelewa mzuri kuhusu mazingira ya kuanzishwa sarafu moja,” anasema Dk. Ndanshau.

Anasema ushindani katika kinyang\’anyiro hicho ni mkali kwa sababu wengi waliojitokeza ni wenye uwezo. Wengi ni madaktari na maprofesa.

”Hiyo ni nafasi nzuri ya ushindani kwa upande wa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa watapata uwakilishi mzuri kwa wale watakaochaguliwa,” anasema Ndanshau.

Kwa mujibu wa Dk. Ndanshau anajiona ana vigezo kwa kuwa ana uwezo wa kuwa mbunge katika Bunge hilo.

Anasema unapokuwa mwakilishi kuna wizara husika ambazo kwa ushiriki wake anaweza kuwashirikisha mawazo yake aliyonayo.

Matarajio yake hatawaangusha Watanzania kwa kuwa atashiriki kikamilifu katika uwakilishi huo endapo atachaguliwa.

Akizungumzia upeo wake kisiasa anasema mpaka sasa ni mwenyekiti wa CCM wa tawi la Abiani Chuo Kikuu cha Mlimani tangu mwaka 2002 mpaka sasa.

Pia amekuwa akishiriki vikao vya chama vya kitaifa, wilaya hata mkoa kwa kutoa michango muhimu katika chama.

Ndashau anasema amekuwa mwanachama wa TANU tokea mwaka 1977, na baada ya hapo alichukua kadi mpya ya CCM mwaka 1994.

Kwa upande wa ajira amekuwa mkuu wa idara ya uchumi chuo kikuu mlimani kuanzia mwaka 2003 mpaka mwaka huu. Ana shahada tatu za UDSM, Diploma ya uhasibu kutoka chuo cha biashara Dar es Salaam.

Mwaka jana Dk. Ndanshau aliingia katika kinyang\’anyiro cha kugombea ubunge katika jimbo la Hai mkoa wa Kilimanjaro ambalo kulikuwa na ushindani wa watu saba kutoka CCM.

Anasema kushindwa katika jimbo hilo hakukumkatisha tamaa ya kuendelea mbele katika kuwatafutia wananchi maendeleo katika nyanja mbalimbali, vile vile alikuwa akizielezea sera za chama cha CCM na malengo yake.

”Kushindwa ama kupata ushindi suala hilo tunaliacha kwa wananchi wenyewe waamue,” anasema Ndanshau.

Anasema endapo atachaguliwa katika nafasi hiyo atatumia muda wake kuwatumikia wananchi waliomchagua kwa kuwa anasema nafasi hiyo ni kama ajira kwake anataka kuwatumikia watanzania.

”Uwezo wangu wa elimu ni silaha tosha ambayo Mungu amenipa. Nitatumia uwezo wangu na elimu yangu niliyoipata kwa ajili yaw engine,” anasema Ndanshau.

Oktaba 29 mwaka huu majina ya wagombea hao yatachujwa na kupatikana wagombea 24 ambao majina yao yatapelekwa kwa katibu wa Bunge, tayari kwa kupigiwa kura na wabunge tayari kwa kupatikana idadi ya wabunge tisa wanaohitajika.

Elimu ya sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne alisoma shule ya sekondari Pugu, kidato cha tano na sita alisoma kama mtahiniwa binafsi katika shule ya sekondari Tambaza.

Elimu ya msingi aliipata katika shule ya Nkwamwatu iliyopo Machame kuanzia darasa la kwanza mpaka la sita. Darasa la saba alisoma shule ya Nkwarungo Uduru Machame.Ana mke na watoto wanne.

Mke wake Amen Ndanshau anampongeza mume wake kwa hatua aliyoichukua kwa sababu ni ya kishujaa, pia ameonyesha kutokukata tamaa.

”Uwezo wa kuwatumikia wananchi anao akiwa kama mchumi na mwana siasa, pia mkereketwa mkubwa. Kama Mungu atamsaidia akashinda hiyo nafasi uwezo anao.

Namtia moyo na kumwambia asikate tamaa,”anasema mkewe Ndanshau.

Aidha wasomi wengine waliowania kinyang’anyiro hicho ni Dk Walid Kabourou kwa tiketi ya CCM na Dk Leny Kasoga wa UDSM kwa tiketi ya chama hicho.

Kwa kuwa mijadala ya Bunge la Africa Mashariki inahitaji watu wenye upeo mkubwa wa kuchambua masuala mbalimbali ya uchumi, siasa, biashara, jamii, sayansi na teknolojia, wasomi waliojikita kugombea wana sema ni muhimu wasomi waingizwe katika Bunge hilo.

Wanasema kuna masuala muhimu ya kujadiliwa hususani muundo wa soko la pamoja, utekelezaji wa sera ya sarafu ya pamoja ya Afrika Mashariki na azma ya kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki.

Kuhusu uundaji wa soko la pamoja kuna umuhimu kwa wasomi kutoa mapendekezo kuhusu namna kila nchi itakavyonufaika na mtengamano wa uchumi.

Mapendekezo muhimu yanayozingatiwa maslahi ya kila mwanachama yatasaidia kuimarisha jumuiya ili kuweza kuchochea maendeleo ya watu wa nchi hizi tatu.

Tayari kamati za kukusanya maoni ya juu ya uundaji wa shirikisho imekwishaundwa hivyo msukumo zaidi itategemea jinsi wasomi watakavyowaongoza wadai wengine katika kutoa maoni ambayo ni endelevu.

Nchini Tanzania kamati inaongozwa na mwanazuoni mahiri Profesa Samwel Wangwe ambaye pia ni mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pande zinazotoa mapendekezo zinatakiwa kuongozwa na nguvu za hoja ambazo zinahitaji fikra pevu na zinazoweka bayana maslahi ya wadau wote, wanasema wasomi waliojikita katika kinyang’anyiro hiki.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.