|
Mwamuzi asimamie vizuri pambano la Simba, Yanga
2006-10-28 07:58:23
Na Mhariri
Macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yataelekezwa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam wakati klabu kubwa zenye upinzani wa jadi, Simba na Yanga zitakapovaana katika mechi ya Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara kesho.
Pambano hilo linatazamiwa kutoa mwanga wa nani anaweza kutwaa taji la ligi hiyo kutokana na ukweli kuwa timu hizo mbili ndio zinafukuzana katika nafasi mbili za juu za ligi hiyo.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 59 wakati Simba inaifuatia ikiwa na pointi 57.
Kwa vyovyote vile kutokana na hali hiyo, pambano hilo litakuwa la vuta nikuvute.
Ushindani huo sasa utafanya timu hizo mbili kuweka nguvu kubwa ili kuweza kushinda mchezo huo.
Maana yake ni presha kubwa kwa viongozi, makocha, wachezaji na mashabiki wa timu zote mbili.
Kutokana na mchecheto wa kuogopa kufungwa, kazi kubwa na ngumu inabaki kwa mwamuzi.
Mwamuzi ndiye mtu muhimu katika pambano hili kutokana na namna atakavyodhibiti mchezo.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa pale mwamuzi atakapoboronga ndipo kunaweza kutoa visingizio kwa mashabiki, viongozi na wachezaji kuharibu mchezo.
Imeshatokea mara nyingi kwa pambano kati ya timu hizi mbili kuvunjika kutokana na visingizio vya waamuzi.
Mfano mwaka 1985 mchezo kati ya timu hizi mbili ulivunjika, katika mchezo huo Yanga ilikuwa inahitaji ushindi wakati Simba ilikuwa inatakiwa kutoka sare ili kutwaa ubingwa.
Mchezo ulivunjika baada ya beki wa Simba, Twalib Hilal kushika mpira na mwamuzi kuamuru penati.
Simba waliweka kwapani mpira na baadaye Yanga ilipewa ushindi wa mezani.
Sasa huu ni mfano wa umuhimu wa TFF kuteua mwamuzi ambaye ni jasiri kuweza kuwa makini katika mchezo huo.
Anahitajika mwamuzi ambaye hatakuwa mwoga kutoa maamuzi ya haki kwa kuzingatia sheria 17 za mpira wa miguu na pia ambaye hatasikiliza presha za mashabiki wa timu hizi mbili.
Imani ni kuwa ikiwa mwamuzi atasimamia kwa haki mchezo huu basi pambano hili litatoa matokeo ya haki na pande zote mbili kuridhika na matokeo.
|