28 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Nani anasema kweli juu ya chanzo cha muungano?
 
2006-10-28 07:59:34
Na Nasser Kigwangallah

Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar ni ushahidi wa kutosha kuwa wananchi wa pande hizi mbili kwa asili, wamekuwa na mahusiano mema na ya kiundugu.

Utekelezaji wa mpango wa kuyaunganisha mataifa haya huru, ulifanywa Aprili 26 mwaka 1964 kwa ushirikiano wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Tanganyika) na Hayati Amani Abeib Karume (Zanzibar).

Kitendo hicho ndicho kilichozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Historia au kiini cha mataiafa haya mawili kuungana, inatazamwa kwa mitazamo tofauti.
Wako watu wanaodai kuwa Muungano ulianza kwa talaka.

Katika madai yao, wao wanasema huko nyuma nchi hizi mbili zilikuwa kitu kimoja na watu wake walikuwa wamoja.

Wanadai kuwa kuja kwa wakoloni ndiko kulikotibua mambo baada ya wababe hao kuligawanya taifa hilo ili kurahisisha shughuli za utawala wao.

Wanazuoni wenye mtazamo huo wa historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wanahesabiwa kuwa ndiyo wenye mapenzi na Muungano na wako tayari kuutetea kwa hali na gharama yoyote.

Lakini kwa upande mwingine, kuna wanazuoni wanaopingana na kundi hilo na ambao wasisitiza kuwa Muungano ulitokana na ndoa ya mwaka 1964.

Hao wanahesabiwa kuwa ni watu ambao hawaupendi Muungano na wanaomba mno uvunjike.
Hali kadhalika kuna kundi la tatu linalodai kuwa Tanganyika na Zanzibar hazijawahi kuwa na uhusiano wowote wa kweli.

Hawa wanasema hakuna cha ndoa wala talaka katika muungano huo, isipokuwa ni matumaini tu ya kuona nchi hizi zinaungana kwa manufaa ya kisiasa.
Historia inasema mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni walikutana nchini Ujerumani na kuligawa Bara la Afrika ili kulitawala.

Hicho ndicho kipindi ambacho makabila yaliyokuwa katika maeneo ambayo mipaka iliwekwa, yalijikutaka yakigawanywa katika nchi mbili tofauti.
Makabila hayo ni pamoja na ya Wamasai, Wakurya, Wanyakyusa na kadhalika.

Pengine hatua hiyo ndiyo inayowasukuma baadhi ya wanahistoria kuamini kuwa muungano ulioizaa Tanzania ulitokana kwanza na talaka.

Lakini kwa vyovyote vile, Muungano huo ni wa kujivunia si tu kwa Watanzania na hata Afrika kwa jumla.

Hata hivyo kwa sasa Muungano umeanza kukumbwa na matatizo ambayo Serikali zote mbili zinaziita kuwa ni kero za Muungano.

Kwa bahati mbaya, watu ambao wamezaliwa katika kipindi cha miaka ya sabini, hawajui kiini cha matatizo hayo.

\”Wengi wetu hatuelewi nini maana ya muungano na matatizo yaliyojitokeza wakati viongozi wetu wakuu wakaamua kuunganisha nchi zao,\” anasema Kulwa Mwanawasa wa Gongo la Mboto.

Lakini la msingi hapa ni kwamba matatizo ya Muungano lazima yajadiliwe tena na kila Mtanzania kwa nia njema ya kuuimarisha.

Kufanya hivyo pia kutasaidia katika kuwaelimisha wale wanaotaka kwa kisingizio chochote kile.

Kwanza, ni nani hasa atafaidika kama Muungano utavunjika. Ni wananchi au viongozi wachache wenye uchu wa kutaka kuongoza.

Dunia nzima imeshuhudia jinsi nchi zilivyojitenga.
Mfano halisi ni zile nchi zilizokuwa za Muungano wa Kisovieti ambazo sasa zinateseka kufuatia tukio la kusambaratika.

Nchi hizo sasa maskini wa kutupwa na hazina umoja wala nguvu kama vile zilivyokuwa zamani.

Dunia pia inashuhudia jinsi nchi tajiri za Ulaya Magharibi zinavyoungana kiuchumi ili kuwa na nguvu kubwa za kijamii, kisiasa na kijeshi.

Yafaa pia tujifunze kutoka Marekani, taifa kubwa lakini linaoundwa na muungano wa nchi 50
Hali kadhalika Ujerumani iliyoungana tena mwaka 1989.

Laiti kama nchi za Afrika nazo zingeungana kama ilivyokuwa imetabiriwa na Marais Kwame Nkrumah wa Ghana, Mwalimu Julius Nyerere na wengine kadhaa Afrika nayo ingekuwa na nguvu za kijeshi, kiuchumi na kisiasa.

Pia isingekuwa katika ufukara na udhaifu ambalo leo inao Nchi nyingi hasa tajiri kabisa duniani leo zinaungana na sio kutengana.

Lakini upo ushahidi kuwa wakoloni walizigawanya nchi za Afrika ili kurahisisha mipango ya kuzitawala.
Wanaotaka Muungano wa Tanzania uvunjike, wanataka kutimiza malengo ya wakoloni ambao waligawa Tanganyika na Zanzibar.

Ni dhahiri kuwa wananchi wengi wa Tanzania, tunapenda kuona Muungano unaendelea na ndiyo maana wanahimiza kuwa jitihada zifanyike kuzitafutia ufumbuzi, kero za Muungano.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.