28 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Taasisi ya Mama Kikwete yatenga mil.200 kusomesha
 
2006-10-28 08:07:03
Na Ikunda Erick

Taasisi mpya isiyokuwa ya kiserikali ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), inayoongozwa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, imetenga Sh. milioni 200, kwa ajili ya kuwadhamini watoto watano kila mkoa kwa Tanzania Bara, watakaochaguliwa kuingia elimu ya sekondari.

Aidha, imetenga Sh. milioni 255, kwa ajili ya kumkomboa mwanamke na mtoto wa kike.

Hayo yalisemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mama Kikwete kwenye hafla ya uzinduzi wa Taasisi hiyo ya WAMA uliofanywa na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

Alisema kuanzia mwakani msaada huo utawasaidia watoto wa kike waliotoka kwenye familia duni au yatima wasiokuwa na walezi wenye uwezo.

Kundi lingine litakalonufaika na Sh. milioni 30 ni vijana wa kike 20 kutoka familia duni au yatima wasiokuwa na walezi ambao watachaguliwa kujiunga na elimu ya chuo kikuu na msaada huo ni kwa miaka mitano.

Alisema Sh.milioni 25 pia zimetengwa kusaidia juhudi za Chama cha Madaktari Wanawake Nchini (MEWATA) za kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa wanawake, ambapo fedha hizo zitasaidia wanawake 1000.

Mama Salma alisema ili kufanikisha azma yao ya kumkomboa mwanamke na mtoto wa kike, WAMA imejiwekea malengo sita kama dira ya kufanikisha kazi ya kuinua hali za kundi hilo.

Aliyataja malengo hayo kuwa ni kutafuta fursa za elimu na kuboresha elimu ya mtoto wa kike katika ngazi zote, kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa wanawake na wajawazito na kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Mengine ni kutetea usawa wa kijinsia katika ngazi zote za elimu, kutafuta fursa za elimu na rasilimali zitakazomkomboa mwanamke kiuchumi na kifikra na kutetea mila na desturi nzuri na kupiga vita zile zilizopitwa na wakati na zinazohatarisha maisha ya mwanamke.

Alisema hiyo ni hatua ya awali na kuwa WAMA wataendelea kubuni programu na miradi ya kudhamini na kusaidia watoto wa kike na wanawake wenye matatizo mbalimbali.

Kwa upande wake Rais Karume alisema kuanzishwa kwa taasisi hiyo na mama Kikwete ni kielelezo cha msimamo na dhamira yake katika kujitolea kuinua maendeleo ya wanawake na watoto wa Tanzania.

Alisema mfano huo wa kujitolea ni mzuri wa kuigwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi ili kuwahudumia na kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kadri ya uwezo wao.

Alisema taasisi hiyo ni fursa nyingine kubwa ya kuongeza nguvu mpya katika harakati za kuwaendeleza wanawake zinazoendeshwa na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Alisema wanawake ni nguvu kazi muhimu kwa Taifa lolote duniani kwa kuwa wapo mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya Taifa.

Alisema pamoja na kuwepo mipango madhubuti ya serikali katika kumuinua na kumuendeleza mwanamke, bado fursa hizo hazijaweza kuwafikia wanawake wote.

Taasisi ya WAMA imesajiliwa rasmi Aprili mwaka huu, ikiwa na Bodi ya Udhamini inayoundwa na wajumbe tisa.

Wajumbe hao ni Mke wa Makamu wa Rais, Bi. Mwanamwema Shein, Mke wa Waziri Mkuu, Bi. Regina Lowassa, Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Sofia Simba, Bi. Hulda Kibacha, Balozi Mwanaidi Sinare, Bi. Blandina Nyoni na Mwenyekiti wa bodi hiyo Mama Salma.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.