|
Mil.400 zimetengwa kujenga kituo cha kufunza wakalimani wa Kiswahili-Nswazugwanko
2006-10-28 08:08:20
Na John Ngunge
Serikali imetenga Sh. milioni 400 kujenga kituo cha kufunza wakalimali ili kukuza lugha ya Kiswahili na kukifanya kuwa bidhaa inayoweza kuingizia pato taifa hatimaye kujenga taswira nzuri ya nchi.
Aidha imetoa changamoto kwa vyombo vya habari kupeleka habari kwa wakazi wa maeneo ya vijijini badala ya kujikita kutoa huduma hiyo katika maeneo ya miji peke yake.
Hayo yalisemwa na Naibu wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Daniel Nswazugwanko baada ya kutembelea vyombo vya habari vya IPP jijini Dar es Salaam jana.
Watu wanaoishi maeneo ya vijijini wana kiu kubwa ya habari lakini wanashindwa kupata magazeti kwa sababu hayapatikani katika maeneo yao kwa urahisi, alisema.
Alisema zamani kulikuwa na magazeti yanayoandika habari za vijijini lakini siku hizi magazeti hayo hayapo na akaomba vyombo vya habari vya sasa kuzima kiu hiyo kwa kupeleka habari vijijini.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha kukuzwa lugha ya Kiswahili, Bw. Nswazugwanko alisema ujenzi wa kituo hicho ni agizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye anataka Kiswahili kikuzwe na kuwa bidhaa itakayoleta pato la taifa na kujenga taswira nzuri ya nchi.
Hili ni agizo la Rais Kikwete, anataka tukuze Kiswahili na kukifanya kuwa bidhaa, naomba mkazo uwekwe katika suala hili, tunahitaji sana watu wa kukuza Kiswahili, alisema na kuongeza, tunataka Kiswahili kifundishwe sambamba na lugha zingine duniani.
Alisema kwa mfano wataalamu wa Kiswahili wanahitajika katika Bunge la Afrika, katika ofisi za Umoja wa Afrika na katika vyuo mbalimbali duniani na kama hatua za haraka hazitachukuliwa mataifa mengine yatateka kazi ya kukikuza Kiswahili na kuifanya kuwa ni yao.
Alisema tayari wizara yake ipo katika hatua za mwisho za kupata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC).
Pia alisema ujenzi wa kituo kama hicho utafanyika mjini Adis Ababa, Ethiopia kwenye makao maku ya ofisi za Umoja wa Afrika.
Alisema tayari eneo la ujenzi wa kituo hicho limekwishapatikana kwa kushirikiana na ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza kwa ujenzi huo.
Pamoja na kukuza Kiswahili pia alitaka juhudi zifanywe katika kukuza utamaduni wa Mtanzania.
Kwa kuanzia tunataka kuanzisha matamasha ya utamaduni yatakayofanyika kimkoa kila mwaka na kutangaza utamaduni wetu, tukifikia hapo tutaweza kuufanya utamaduni kuwa ni bidhaa inayoweza kuuzika nje na kupata fedha za kigeni, alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi alimshukuru Naibu Waziri Nswazugwanko kwa ziara yake na akasema amefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kwa vyombo vya habari.
Alimwomba Naibu Waziri huyo asichoke kutembelea vyombo vya habari mara kwa mara.
Katika vyombo vya habari vya IPP, Naibu Waziri Nswazugwanko alitembelea studio za radio za Radio One, Sky Fm, East Africa Radio na studio za televisheni za ITV, EATV, na Pulse Africa.
Kwa upande wa magazeti Bw. Nswazugwanko alitembelea ofisi za The Guardian Ltd ambayo huchapisha magazeti ya The Guardian, Nipashe, Nipashe Jumapili, Sunday Observer, Financial Times, Alasiri na Lete Raha.
|