|
Meya atishia kufunga mnada wa vipuri
2006-10-28 08:09:53
Na Joseph Mwendapole
Meya wa Manispaa ya Ilala, Bw. Abuu Juma, ametishia kuufunga mnada wa vifaa vya magari ulioko eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kutokana na kuhatarisha usalama wa watu.
Bw. Jumaa aliyasema hayo jana baada ya kutembelea mnada huo na kukuta msongamano mkubwa wa vibanda ambavyo vimebanana.
Alikuwa katika ziara ya siku moja ya kukagua hali ya usafi maeneo mbalimbali ya katikati ya Jiji, kufuatia bomoabomoa iliyofanyika hivi karibuni.
Alisema endapo moto utazuka eneo hilo, watu waliomo watateketea na mali zao kutokana na kutokuwepo kwa nafasi za kutosha kwa ajili ya wapita njia.
Alisema mbali na hatari ikiwa utazuka moto, uchafu wa kupindukia unaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Alisema kutokana na msongamano mkubwa, wenye vibanda hivyo wamekuwa wakishindwa kukaa ndani na kulazimika kukaa nje kupunga hewa.
Nilishawaambia mbadilike lakini kwa muda mrefu hamtaki sasa kitakachofuata ni kufunga kabisa biashara maana hali hii si nzuri kwa afya na usalama wa watu, alisema.
Alisema baada ya zoezi la kubomoa vibanda maeneo yaliyojengwa kinyume cha sheria, maeneo mengi yamekuwa safi isipokuwa eneo hilo.
Akijitetea, Mwenyekiti wa soko hilo, Bw. Hamis Zwangi, alisema katika kipindi cha miezi miwili watakuwa wamejenga jengo la kisasa hivyo hakutakuwa na msongamano kama huo.
Mheshimiwa, ukija hapa miezi miwili ijayo hutakuta uliyoyaona leo maana tayari mpango wetu wa kujenga jengo la kisasa umekamilika, alisema.
Baada ya kupata maelezo hayo, Bw. Jumaa aliuagiza uongozi wa soko hilo kumpelekea maelezo ya kina kuhusu ujenzi wa jengo jipya.
Nataka Jumanne mje mnieleze kwa kina nione kama kuna azma ya kweli ya kufanya mabadiliko la sivyo tutafunga...hapa hatukumoani ila tunataka kuokoa maisha ya wengi, alisema.
|