|
Ajinyonga chumbani kwa khanga
2006-10-28 08:10:50
Na Romana Mallya
Mkazi wa Bunyokwa B Mavurunza, Dar es Salaam, Theopard Thadeu (25), amekutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia upande wa khanga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana eneo la Bunyokwa B, Mavurunza ambapo mwili wake ulikutwa ukiwa unaninginia juu ya kenchi katika chumba alichokuwa akiishi.
Kamanda Rwambow alisema kwa mujibu wa majirani zake, marehemu enzi za uhai wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa akili.
Alisema mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio lingine, fundi ujenzi aliyefahamika kwa jina moja la Ibrahim, amekufa wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kudondoka kutoka kwenye paa la nyumba aliyokuwa akijenga.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Bw. Masindoki Masindoki alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana katika eneo la Gongo la Mboto.
Kamanda Masindoki alisema kwa mujibu wa mtoa taarifa polisi, Bw. Justine Ndubuga (38) ambaye ni mkandarasi wa nyumba hiyo, fundi huyo baada ya kuanguka, alizimia na kukimbizwa hospitali ya Taifa Muhimbili lakini alikufa siku iliyofuata.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio lingine, nyumba yenye vyumba sita imeteketea kwa moto pomoja na mali zote zilizokuwemo.
Kamanda Rwambow alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana katika eneo la Msasani Mikoroshini na kwamba nyumba hiyo ni mali ya Bw. Seleman Yassin (64).
Alisema moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zima Moto cha Halmashauri ya Jiji ambapo chanzo na thamani ya mali zilizoteketezwa bado hazijajulikana.
|