28 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mpasuko wagawa viongozi Z’bar
 
2006-10-28 08:12:27
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Suala la mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar, limeanza kuwagawa viongozi wa kambi ya upinzani ambapo wakati baadhi yao wanataka kuundwa kwa Serikali ya mseto, wengine wanapinga.

Msuguano huo umekuja baada ya viongozi wa chama cha NLD kutishia kwenda mahakamani kupinga serikali yoyote ya umoja wa kitaifa itakayoundwa Zanzibar kwa madai kuwa hatua hiyo itakuwa ni kinyume cha Katiba ya Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa NLD, Bw Rashid Ahmed Rashid, alisema uchaguzi mkuu wa Zanzibar umemalizika na kuendelea kuhoji serikali iliyopo madarakani ni kinyume na uamuzi wa wananchi walioichagua.

Lakini Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw Ambari Khamis kwa upande wake, alisema hakuna njia ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar zaidi ya Wazanzibari kukaa pamoja na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Bw Khamis alisema kutokana na tofauti za kisiasa zilizopo Zanzibar, kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo kutaleta maelewano miongoni mwa wananchi.

”Serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo suluhisho la matatizo ya kisiasa Zanzibar na kukataa kuunda serikali hiyo ni kujidanganya kwa vile Zanzibar ina matatizo makubwa ya kisiasa,” alisema Bw. Ambari.

Alisema madai ya uchaguzi kuwa huru au kutokuwa huru ni mitazamo ya vyama vya siasa, lakini ukweli ni kwamba Zanzibar kuna matatizo na njia ya kuyamaliza ni wananchi wote kushiriki katika serikali yao.

Katibu Mipango na Uenezi wa TADEA, Bw. Juma Ali Khatib, alisema viongozi wa upinzani wanaopinga kuundwa kwa serikali ya mseto, hawana uchungu na ustawi wa Zanzibar kisiasa na kiuchumi.

Alisema tangu kuibuka kwa matatizo ya kisiasa Zanzibar, wananchi wamekuwa wakirudi nyuma kimaendeleo kutokana na hali mbaya inayoikabili Zanzibar na kutumia muda mwingi kuzungumza siasa badala ya kujenga nchi.

”Wanaopinga juhudi za Rais Kikwete kuleta maelewano ya Wazanzibari, hao hawana uchungu na Zanzibar, kwa vile hakuna njia ya kuondoa matatizo yaliyopo zaidi ya kukaa pamoja,” alisema Bw Khatib.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa UPDP, Bw. Haji Othman alisema matatizo ya Zanzibar yanahitaji kujadiliwa kwa umakini kabla ya kufikiwa muafaka.

Alisema hatua za kisiasa zilizofikiwa katika siku za nyuma zinashindwa kufikia malengo katika utekelezaji kutokana na kuwepo watu katikati wanaoamini kuwa wana haki kuliko Wazanzibari wengine.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Bw Seif Sharif Hamad alisema inashangaza viongozi wanaoipinga hatua za Rais Kikwete kuleta maelewano vyama vyao havina ofisi wala wanachama Zanzibar.

Alisema viongozi hao wanatetea maslahi binafsi na kuweka kando maslahi ya wananchi walio wengi.

”Hao wanaopinga juhudi za Rais Kikwete kuleta maelewano miongoni mwa Wazanzibari wanazingatia maslahi binafsi kwa vile vyama vyao havina hata matawi wala wanachama Zanzibar,” alisema Bw Hamad.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Bw. Vuai Ali Vuai alisema CCM bado haijatoa tamko juu ya mpasuko wa kisiasa, kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

”Tumpe nafasi Rais Kikwete kama alivyosema mwenyewe kuwa anashughulikia suala hilo, lakini sisi kama chama hatujatoa tamko lolote hadi sasa,” alisema Bw. Vuai.

Mjadala mkali juu ya serikali ya mseto Zanzibar umeibuka tangu Rais Kikwete kutumia siku tano za mapumziko Zanzibar na kukutana na wanasiasa mbalimbali, tukio ambalo wengi walitabiri ni katika juhudi za kushughulikia mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.