|
Basi lateketea
2006-10-28 08:13:28
Na Nashon Kennedy, Mwanza
Basi la Kampuni ya Mohamed Trans, limeteketea kwa moto katika eneo la Buhongwa, wakati likiwa njiani kutoka Mwanza kuelekea Kahama, mkoani Shinyanga. Lilikuwa na abiria 60.
Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa kwenye msafara wa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, alishuhudia wananchi pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, wakijaribu kuzima moto huo bila mafanikio.
Moto huo ulianza saa 7:00 mchana na kudumu kwa dakika 15, ambapo askari wa kikosi cha zimamoto kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walifika katika eneo la tukio kusaidia kuuzima moto huo.
Hata hivyo, jitihada hizo hazikufanikiwa na basi hilo likateketea.
Dereva na kondakta, ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja, walitoweka.
Hata hivyo, abiria wote 60 walinusurika na chanzo cha moto huo, hakikuweza kujulikana.
|