28 Oct 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Machinga marufuku Mitaani - Lowassa
 
2006-10-28 08:14:55
Na Edward Lowassa

Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jiji na Manispaa, kuhakikisha kuwa wachuuzi wa biashara ndogo ndogo, maarufu kama Wamachinga, hawarudi tena kwenye maeneo walikoondolewa hivi karibuni.

Waziri Mkuu pia ameagiza kuwa, maeneo yaliyobomolewa vibanda vya biashara vya Wamachinga, yasafishwe na kupandwa miti au maua kuboresha mandhari na yasiwe kivutio tena kwa waliohamishwa kurudi na kwamba kampeni ya kuliweka jiji safi, iendelee kwa kasi kubwa zaidi.

Alitoa maagizo hayo katika barua yake kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jiji na Manispaa tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke, kuwapongeza kwa kufanikisha zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo katika maeneo yasiyohusika na kupangiwa maeneo maalum.

Alisema wananchi wengi wa Dar es Salaam, sasa wanaona manufaa ya kutekelezwa kwa zoezi hilo kwa kuwa barabara sasa ni wazi zaidi na hivyo kupunguza msongamano na vile vile kazi ya kuweka Jiji katika hali ya usafi sasa ni rahisi zaidi.

”Kukiwepo na uongozi wa pamoja, umakini na wananchi wakielimishwa watambue faida za hatua mbalimbali za serikali, hakuna ulazima wa kutumia nguvu katika kutekeleza majukumu …hata yale magumu kama hilo la kuwaondoa wananchi wanaokiuka sheria na kanuni za uendeshaji miji,” alisema.

”Uongozi wa mkoa umefanya kazi hii kwa pamoja na kama timu moja. Mmewaelimisha wananchi na mmewaondoa kwa ustaarabu mkubwa sana.

Wapo waliokuwa wana hofu kutokea fujo katika utekelezaji wa kazi ya kuwaondoa wafanyabashara ndogondogo,” aliongeza.

Lakini, Waziri Mkuu aliwaonya viongozi hao kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hawarudi tena kwenye maeneo hayo na mengine ambayo hayakutengwa kwa matumizi ya biashara ndogo ndogo.

”Mshirikiane na wataalamu wa Mipango Miji ili maeneo yale yaliyobomolewa yasafishwe na yapandwe miti au maua ili kuboresha mandhari ya jiji na yasiwe kivutio cha watu kutaka kurudi tena kwenye maeneo hayo,” alisema.

Aliongeza: ”kampeni ya kuweka jiji katika hali ya usafi iendelee kwa kasi kubwa zaidi…Nawapongeza tena na kuwataka muendelee kwa ari na kasi hiyo mliyoionyesha”.

Maelfu ya wafanyabiashara ndogo ndogo mapema mwezi huu waliondolewa katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa biashara hiyo na kupelekwa kwenye maeneo maalum yaliyopangwa katika zoezi lililofanikiwa, ambalo halijapata kutokea katika historia ya jiji la Dar es Salaam.

Mwezi Machi mwaka huu, Waziri Mkuu alitoa miezi sita hadi Septemba 30, kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jiji na Manispaa tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke, kuhakikisha kuwa wanawaondoa wafanya biashara ndogondogo waliozagaa ovyo na kuwahamishia kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.