01 Nov 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Jengo hili liwe la machinga kweli
 
2006-11-01 08:47:38
Na Mhariri

Ni faraja kubwa kusikia kwamba serikali ina mpango wa kujenga jengo la kisasa kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa, jengo hilo la kisasa litakalogharimu shilingi bilioni 10, litajengwa katika eneo la makutano ya barabara za Lindi na Kawawa, nyuma ya uwanja wa michezo wa Karume wilayani Ilala.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wafanyabiashara wapatao 10,000 wataweza kufanya shughuli zao bila bughudha na kwamba jengo hilo litakuwa kivutio kikubwa cha utalii kutokana na jinsi litakavyojengwa ambapo barabara zilizotajwa zitapita chini ya jengo hilo.

Ujenzi utakaogharimiwa na Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwakani na kukamilika ndani ya miezi kumi.

Hiyo ina maana kwamba kati ya Oktoba na Novemba mwakani, wamachinga watakuwa wanaendesha biashara zao katika eneo hilo la kisasa.

Tunachukua fursa hii kuipongeza Serikali na wadau wote kwa kuchukua hatua hii ambayo tunaiona inaweza kuwa mwisho wa tatizo la miaka mingi la kulundikana kwa wamachinga katika maeneo yasiyo rasmi katika jiji la Dar es Salaam.

Bila shaka, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, sokomoko kati ya wamachinga na askari sasa itakuwa historia.

Lakini tunapenda kutoa tahadhari moja, kwamba jengo hilo liwe kwa ajili ya machinga na sio vinginevyo.

Tunasema hivi kwa sababu ya uzoefu wa miaka ya karibuni ambapo masoko mazuri yalijengwa katika jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, lakini kwa mshangao wa kila mtu, meza za masoko hayo wakapewa watu wengine ambao si wafanyabiashara wadogo na kupewa watu wengine ambao si walengwa.

Aidha kodi kubwa ya kupanga katika masoko hayo ikawa sababu nyingine ya wafanyabiashara kushindwa kufanya shughuli zao katika masoko hayo.

Baadhi ya masoko hayo ni lile la Temeke Stereo na Makumbusho. Matokeo yake ni kwamba masoko hayo yamekuwa hayatumiki kwa kiwango kilichotarajiwa kutokana na sababu hizo.

Hatutarajii kuwaona wakubwa wakigawana sehemu za biashara katika jengo hili la kisasa linalotarajiwa kujengwa. Itakuwa dhambi kujenga jengo hilo kwa kutumia jina la machinga halafu baada ya kukamilika wanaopata nafasi si machinga bali vigogo na matajiri.

Hata hivyo tuna imani Serikali haitakubali kuona watu wachache wenye uroho wanapindisha madhumuni ya ujenzi wa soko hilo ili wafanyabiashara ndogo ndogo nao wanufaike kupitia serikali yao.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.