|
Wachezaji Yanga walalamikia maandalizi
2006-12-20 08:56:27
By Jimmy Charles
Wachezaji wa timu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam,wamesema ni ndoto kwa timu hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama kombe la Kagame inayotarajia kuanza Januari 6 nchini Rwanda, kama hakutakuwa na maandalizi ya kutosha.
Akizungumza na Nipashe jana, mlinda mlango namba moja wa timu hiyo, Ivo Mapunda, (pichani) alisema kuwa ili kupata mafanikio katika mashindano yeyote ni lazima maandalizi ya kutosha yafanyike.
Ukweli ni kwamba viongozi wetu wasitarajie miujiza katika mashindano makubwa kama haya, hadi sasa hatujaanza maandalizi yeyote unafikiri tutafika mbali kweli ikiwa wenzetu wako katika maandalizi ya michuano hiyo, alisema Ivo.
Ivo alitoa wito kwa viongozi wa klabu hiyo kuhakikisha muda huu mfupi uliobaki wanautumia kwa kuwaweka kambini ili kupata mafunzo ya pamoja yatakayowasaidia kuzoeana zaidi.
Nae mmoja wa washambuliaji mahiri wa timu hiyo, ambae alikataa kuandikwa jina lake gazetini alisema kuwa uzembe unaofanywa na uongozi wao utasababisha pia kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa inayowakabili.
Mchezaji huyo alisema kuwa viongozi wao wanataka timu ipate mafanikio bila kujua mafanikio hayo yatapatikana kwa namna gani viongozi wetu wanapenda sana timu ipate mafanikio lakini hawajui ni jinsi gani wafanye ili kuleta mafanikio hayo, alisema mchezaji huyo.
Alisema kuwa ni suala la busara kama uongozi utawaweka pamoja ili kujumuika na wachezaji wapya waliosajiliwa hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jack Chamangwana alisema kuwa kushindwa kuingia kambini mapema kutawaathiri wachezaji wake ambao wengi wao ni wapya.
Aidha uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa utaiweka timu kambini mapema mwezi Januari lengo likiwa ni kupisha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Timu ya Yanga katika michuano ya Kagame imepangwa kwenye kundi C ikiwa na timu za Benedir, Eritrea na Polisi Uganda ambayo itaanza nayo.
|