|
TFF imeboronga suala la Athumani Idd - Mziray
2006-12-21 08:22:59
By Somoe Ng’itu
Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Syllersaid Mziray, amesema kuwa shirikisho la mchezo huo nchini (TFF) limechemsha kumbana mchezaji, Athumani Iddi kwa kutumia mkataba wake na Simba.
Akizungumza jana asubuhi katika kipindi cha michezo cha redio One, Mziray alisema kuwa TFF na Athumani hawapaswi kujadili mkataba wa miaka mitatu unaodaiwa kusajiliwa kwenye shirikisho hilo kutokana na soka la Tanzania kuwa la ridhaa na sio la kulipwa.
Alisema kuwa TFF wanaposema kuwa mchezaji huyo ana mkataba na klabu ya Simba ni kupingana na sera ya michezo ya nchi ambayo inatambulika kuwa michezo yote ni ya ridhaa na kwa upande wa soka mchezaji humaliza mkataba na klabu pale msimu unapomalizika.
TFF imechemka katika maamuzi yake na Athumani Iddi habanwi na mkataba kwa kufuata sheria za nchi labda watangaze mabadiliko na kusema kuwa soka tena si la ridhaa hapa nchini, alisema.
Alisema pia katika hali ya kawaida mchezaji huyo akibaki Simba hatacheza vizuri kutokana na kutokuwa na mapenzi tena na klabu hiyo kwa sababu soka la sasa hivi linachezwa kwa kufuata maslahi na si mapenzi kama ilivyokuwa hapo zamani.
Hii yote imetokana na klabu za Simba na Yanga kutumia ulaghai mwingi katika usajili na si fedha, aliongeza.
Yanga na Simba zimemtangaza kumsajili mchezaji huyo kwa ajili ya msimu ujao lakini TFF imesema kuwa inatambua kiungo huyo ni wa Simba kutokana na kuwa na mkataba wa miaka tatu uliosajiliwa kwake.
|