|
Chamangwana ateremshwa cheo Yanga
2006-12-21 08:23:58
By Renatha Msungu
Kufuatia ujio wa makocha wawili wa mabingwa wa soka nchini, Yanga, kutoka nchini Poland,kocha mkuu wa timu hiyo, Jack Chamangwana ameteremshwa cheo na sasa atafundisha timu za vijana wadogo wa timu hiyo.
Chamangwana, ambaye ni raia wa Malawi, kwa nafasi hiyo ndio atahusika na kuandaa timu ya yosso itakayoshiriki kwenye mashindano ya Copa Cocacola yanayoshirikisha timu za vijana wadogo.
Akizungumza na Nipashe jana, Kiongozi mmoja wa juu wa Yanga, alisema, hata hivyo, katika kipindi kabla ya kuanza mashindano ya Yanga atakuwa katika benchi la ufundi katika kusaidia kunoa timu ya wakubwa.
Alizidi kufafanua zaidi ya kuwa Chamangwana hawezi kuachwa kama inavyodaiwa, isipokuwa nafasi yake itabakia ya ukocha ila kwa timu za yosso.
Chamangwana ni kocha aliyetupa mafanikio, sasa kwanini tumuache, alihoji kiongozi huyo.
Wakati huo huo, makocha wawili wa kigeni ambao wanatarajia kuingia mkataba na Yanga, wanatarajia kuwasili nchini kati ya Januari 6 na 7 kutoka Poland.
Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa Yanga, alisema makocha hao wakifika, wataanza mara moja mazoezi ya kuinoa timu hiyo, huku wakiwa na mwenyeji wao Chamangwana.
Chamangwana atakuwa nao kwa muda akiwazoesha mazingira ya hapa pamoja na timu, baada ya hapo, ataendelea na maandalizi ya timu za vijana, alisema.
Chamangwana, toka amejiunga na Yanga mwishoni mwa mwaka 2004, ameiwezesha kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo. Pia alifundisha timu hiyo mwaka 2002.
|