|
Wachezaji waache unafiki - Yanga
2006-12-21 08:24:46
By Renatha Msungu
Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga umewashutumu wachezaji wa timu hiyo kwa kutoa madai waliyoyaita ya kinafiki ya kutaka waanze mazoezi mapema.
Kiongozi wa ngazi ya juu ya klabu hiyo, aliwatuhumu wachezaji hao mara nyingi walikuwa wakiitwa kwenye mazoezi wakati wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, walikuwa wakitoroka na kwenda kucheza mechi za mchangani.
Wachezaji wetu hawa wanakuwa vigeugeu, sababu ukiwaita katika mazoezi ya ligi ya nyumbani wanakacha na kukimbilia kwenye ligi za mchangani, alisema.
Alisema Yanga wameamua kuchelewa kuanza mazoezi, kutokana na ushauri waliopewa na wataalamu wa soka wa kutakiwa wachezaji wapumzike baada ya msimu mrefu wa ligi.
Unajua hata kocha wa timu ya taifa, Marcio Maximo, alitushauri kuwa wachezaji wapumzike ili waanze msimu mpya vizuri, alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alisema pia kambi hiyo imeshindikana kuanza kutokana na wachezaji hao kupewa ruhusa ya kwenda mikoani kwao, kucheza kwenye kombe la taifa.
Hata hivyo, kiongozi huyo amesema, wachezaji wametakiwa kuripoti mazoezini mara baada ya sikukuu za Krismas na mwaka mpya, kwa ajili ya mazoezi ya maandalizi ya michuano ya kombe la Kagame yaliyopangwa kuanza mapema Januari 6 nchini Rwanda.
Kauli hiyo imekuja baada ya wachezaji wa Yanga kukaririwa na gazeti hili jana wakilalamika kuwa hawataweza kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Kagame kutokana na kuchelewa kuanza mazoezi mapema.
Yanga imepangwa katika kundi la C, ikiwa na timu za Polisi ya Uganda na Benedir ya Eritrea.
|