21 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Amekidhi matumaini ya Watanzania?
 
2006-12-21 08:48:14
Na Mwandishi Wetu

Ni Mwaka mmoja sasa tangu Jakaya Mrisho Kikwete aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzanika, baada ya kushinda kwa kishindo, au kimbunga kama wana CCM wenyewe anavyopenda kusema, katika uchaguzi mkuu mwaka 2005, kwa kupata asilimia zaidi ya 80 ya kura za Urais.

Katika uchaguzi huo chama chake, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilishinda kwa kishindo pia katika ngazi zote za mitaa, udiwani na ubunge.

Pamoja na malalamiko ya baadhi ya watu na vyama vingine vya siasa kwamba palikuwa na wizi wa kura na udanganyifu katiba baadhi ya sehemu, asilimia kubwa ya Watanzania, pamoja na baadhi ya wanachama wa vyama vingine, walikubali kuwa Kikwete na chama chake walipata ridhaa kubwa ya Watanzania kuongoza nchi.

Ishara ya ushindi kwa Kikwete na Chama Cha Mapinduzi vilianza kuonekana mara baada ya uteuzi wake kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM.

Wachache watakataa kuwa Kikwete anamvuto wa kipekee na ameiongezea hadhi na heshima CCM, ambayo ndiyo iliyomlea na kumfikisha hapa alipo. Naye anakiri hivyo.

Kwa hiyo kwa kuchaguliwa kwake na umma wa Watanzania na kwa kauli mbio yake ya Nguvu mpya, Ari mpya na Kasi mpya, Rais Kikwete aliwapa Watanzania matumaini mapya na makubwa. Matumaini ya maendeleo makini, ya haraka na maisha bora zaidi.

Siyo hivyo tu, ilani ya uchaguzi ya CCM nayo ilisheheni ahadi kem kem za kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwaletea maendeleo katika kila fani ya maisha, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kwa maoni ya wachambuzi wengi wa kisiasa, ahadi kubwa ya kiuchumi aliyotoa Rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi na kurudia baada ya kuapishwa ni kutoa ajira mpya milioni moja katika awamu yake ya kwanza ya miaka mitano.

Aidha, Rais Kikwete na chama chake cha CCM waliahidi kuboresha huduma za kijamii kama vile shule, hospitali, barabara na maji.

Kisiasa, Rais Kikwete aligusa tatizo gumu na la miaka mingi la hali ya Muungano na mgawanyiko wa Watanzania wa Zanzibar.

Rais Kikwete aliahidi kusimamia kuondolewa kwa kero za Muungano ambazo zimekuwa zikisababisha woga wa kuvunjika kwake na kusimamia amani ya kudumu kwa watu wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa kauli mbiu yake na kwa ahadi zake na za chama chake, Raisi Kikwete alijiwekea mtihani mgumu sana wa kutekeleza ahadi hizo na kukidhi kiu ya maendeleo na ya ubora wa maisha ya Watanzania.

Sasa, swali linaloulizwa na baadhi ya watu ni kwa kiasi gani ahadi hizi zimetekelezwa au zimeshindikana kutekelezwa.

Kuna baadhi ya watu wanaamni kuwa mwaka mmoja hautoshi kupima mafanikio ya ahadi hizi ukizingatia ukubwa na uzito wa suala lenyewe, ukubwa wa nchi yenyewe, ugeni wa uongozi huo wa juu, uchanche wa rasilimali na uduni wa teknolojia ya kutumia rasilimali iliyoko, na majanga ya asili yaliyoikumba nchi yenyewe katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa uongozi wake.

Kwa kipimo cha binadamu, mwaka mmoja ni umri wa mtoto kusimama na kuanza tutembea.

Lakini kiuchumi na kijamii mwaka mmoja unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika nchi.
Lakini kwa hakika siamini kuwa mtu au watu walitegemea kuona mabadiliko makubwa katika kila sekta.

Ni wazi kuwa kila moja angependa kuona mabadiliko katika fani fulani ambayo pengine inahusiana na misha yake mmoja kwa mmoja.

Pengine siyo rahisi vile vile kuona mafanikio ya wazi katika sekta yoyote ile katika muda wa mwaka mmoja.

Kwa kifupi, Rais Kikwete aliorodhesha mafanikio mengi alipolihutubia taifa siku ya kusherehekea miaka 45 ya uhuru wa nchi hii.

Naamini hapana haja ya kurudia orodha hiyo, lakini ni muhimu kusema hapa kuwa, nia ya kutekeleza mambo aliyoahidi kuyafanya imeonekana wazi.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.