|
ZFA yagawanyika kutimuliwa kwa Bushiri
2006-12-22 08:49:56
By Somoe Ng’itu
Chama cha soka Zanzibar (ZFA) kinadaiwa kufanya maamuzi ya kumtimua Ali Bushiri kama kocha msaidizi kwenye timu ya Tanzania (Taifa Stars) kwa sababu ya chuki na kuwa jambo hilo halikujadiliwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya chama hicho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na katibu mkuu wa ZFA, Mzee Zam Ali inasema kwamba maamuzi hayo yalifikiwa na kamati ya utendaji ya chama hicho kuwa Bushiri pamoja na daktari wa timu, Abdulla Said Mohammed hawakuwa na nidhamu.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, mmoja wa viongozi wa chama hicho alisema kuwa kutolewa kwa taarifa hizo kumefanywa na baadhi ya wajumbe ambao wanaonekana kutokuwa na mawasiliano mazuri na kocha huyo.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa hata taarifa rasmi ya kocha huyo kuondolewa kwenye timu ya Zanzibar bado hajapewa na hiyo inatokana na utata uliojitokeza ndani ya wajumbe wa kamati ya utendaji kuhusiana na kiwango cha juu alichokuwa nacho Bushiri.
Kwa kweli suala la kumuondoa kwenye timu ya Taifa Stars halikujadiliwa ila kwa timu yetu ya Zanzibar ndio lilifikiwa maamuzi ya kumuondosha, alisema kiongozi huyo.
Wakati huohuo, Bushiri aliliambia Nipashe jana kuwa amekubali maamuzi ya viongozi wa ZFA kumtimua kwenye timu ya visiwani lakini hawana ubavu wa kufanya hivyo katika kikosi cha Stars.
Bushiri alisema kuwa makubaliano yaliyokuwa yanafikiwa kati ya shirikisho la soka nchini (TFF) na ZFA sasa yamebadilika tangu kuwasili kwa kocha, Marcio Maximo na kuongeza kuwa Mbrazil huyo atakuwa anasaidiwa na kocha anayeona kuwa anafaa.
|