|
Kasambala aingia mitini Prisons
2006-12-23 08:26:42
By Jimmy Charles
Mchezaji wa timu ya soka ya Prisons ya Mbeya Wajelajela, Pius Kasambala, ambae ametangazwa kusajiliwa na timu ya soka ya Simba, amedaiwa kutoweka kambini .
Akiongea na Nipashe jana, Afisa michezo wa jeshi la Magereza, Twalib Twalib, alisema kuwa mchezaji huyo ambae ni muajiriwa wa jeshi hilo ametoweka kwenye kituo chake cha kazi na haijulikani amekwenda wapi.
Twalib alisema kuwa Kasambala, ambaye analitumikia jeshi hilo mkoani Mbeya na mara baada ya kutoweka kambini taarifa zilipelekwa moja kwa moja kwao.
Pius Kasambala ametoweka kambini kwake na hadi sasa hivi hatujui yuko wapi na hatuna taarifa nae,sisi bado tunajua ni mfanyakazi wetu halali hadi pale mkuu wa jeshi litakapoamua vingine,alisema Twalib.
Twalib alisema kuwa Kasambala ametoweka kambini toka Desemba 11 na toka alivyoondoka hajaonekana tena,alisema kuwa kwa mujibu wa sheria za jeshi la magereza mchezaji huyo atatambulika kama muajiriwa hadi pale atakapopatikana ndipo hatua nyingine zitachukuliwa.
Aidha Twalib aliongeza kuwa Kasambala anajipotezea muda wake kwani ni vigumu kuikimbia serikali ni vema kama angeamua kuvunja mkataba na muajiri wake kwa kufuata taratibu zote za sheria ya mkataba wake.
Hazuiliwi kujiunga na timu au kazi yeyote,cha msingi ni kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na muajiri wake kwenye mkataba aliousaini yeye mwenyewe, alikuwa na uwezo wa kusitisha mkataba wake na jeshi la magereza,aliongeza Twalib.
Kwa mujibu wa taratibu za mkataba wa jeshi la magereza ,kama itabainika mchezaji huyo amevunja mkataba atakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Kasambala ni mmoja kati ya wachezaji sita waliotangazwa kusajiliwa kwenye kikosi cha timu ya Simba itakayoshiriki kwenye michuano ya kombe la Shirikisho,wachezaji wengine ni Mohammed Banka (Yanga), Moses Odhiambo (Moro United), Zahir Mlawa (Transit Camp), Joseph Kaniki na Josephat Oyando kutoka Tusker ya Kenya.
|