|
Vijana vijiweni wanataka kujinasua lakini...
2006-12-24 09:55:47
Na Anti Flora Wingia
Yupo kijana mmoja nilikutana naye wiki hii eneo fulani nikipata soda. Alikuwa na mwenzake wakimsubiri mwenzao mwingine aliyechepuka kidogo kwenda sehemu fulani.
Mmoja wa vijana hawa akapokea simu. Katika mazungumzo akawa anaambiwa asubiri hadi Januari mwakani ndipo atapata jibu zuri kuhusu mafunzo anayotaka kuchukua.
Baada ya kumaliza simu, huku nikiwa nateta na bibie mmoja rafiki yangu, kijana huyu akanisogelea kutaka kunifahamu. Hiyo ni baada ya kusikia kuwa mimi ni mwandishi wa habari.
Anti afadhali nimekuona na naamini utanisaidia. Natafuta kazi kukidhi maisha lakini zifanikiwi. Sisi vijana tumepuuzwa sana na kila tukijitahidi inashindikana, hivi ndivyo alivyoanza kusema kijana huyu.
Akaendelea, nimeamua nijiunge jeshi la polisi...nimeomba lakini nasubiri majibu. Ila nina mashaka ya kukubaliwa kwa sababu nina mchoro wa tatoo mikononi na nimefikiria alama hizi nipige sindano ya ganzi, kisha nizichome kwa pasi ya umeme ili pawe jeraha zifutike lakini rafiki zangu wananikataza.
Kwanza hata mimi nafikia mahali nahofu kwani sijapima ukimwi nisije kujitia majeraha halafu nisipone. Hata hivyo, yupo jamaa yangu ananiunganishia huko chuoni na amenitaarifu nisiwe na wasiwasi.
Pia nahofu tatoo hizi zaweza kuchukuliwa kama signal ya kundi fulani baya hivyo kuachwa katika kuchaguliwa.
Hata hivyo, kama sitafanikiwa, nitatafuta pasipoti nitokomee nchi za nje kwani maisha ya hapa siyawezi, anasema kijana huyu anayeonyesha kukata tamaa kimaisha.
Nilipomchunguza haraka haraka, niligundua kuwa ni kijana anayejua mambo mengi sana hasa yanayofanywa na rika lake. Aligusia mbinu wanazotumia vijana kununua, kuuza na hata kutumia madawa ya kulevya. Pia aligusia vitendo vya ujambazi.
Akasema, serikali bado iko gizani kuhusu vijana. Rika hili linafahamu mambo mengi ya mitaani.
Na kwa maelezo yake, nia yake ya kujiunga jeshi la polisi ni baada ya kuona mambo ambayo angeyashughulikia akibahatika kuwa ndani ya chombo hicho kwa sababu anayafahamu.
Alitoa mfano wa vijana na madawa ya kulevya. Kwamba katika vijiwe vyote hapa Jijini Dar es Salaam anavifahamu. Lakini anasema hadi hapo serikali itakapompa ajira ndipo atakuwa mstari wa mbele kufichua.
Kwa maelezo yake anajua wapi dawa hizo zinapatikana, zinakouzwa, bei zake, waliko watumiaji wake na kadhalika. Hata baadhi ya vijana majambazi anawafahamu.
Mfano majambazi wawili kati ya waliohusika na wizi mkubwa wa fedha uliosababisha mauaji eneo la Ubungo anawafahamu.
Kijana huyu katika kumsikiliza, nilijawa na mawazo mengi sana.
Kwanza ni kijana mwenye matumaini makubwa ya kuishi. Ni mjanja na mwenye kutaka kujiendeleza lakini anakosa mfadhili.
Ni kijana aliyepitia maisha ya vijiweni na sasa anataka kujinasua lakini kwa namna gani ndiyo kitendawili kikubwa kwake.
Huyu ni kijana mmoja kati ya wengi wanaotaka kubadili mfumo wa maisha.
Ukiona wanalilia ajira baada ya kuelea vijiweni ambako wamebaini hakuna manufaa mbali na kuharibikiwa, basi ujue wamejifunza mengi.
Serikali kupitia vyombo vyake iligeukie kundi hili. Ishirikishe asasi za kiraia kuweka programu za vijana kuona namna ya kuwasaidia. Siyo kuelekeza nguvu au tuseme mapambano kwenye maeneo mengine kama ukimwi, walemavu na yatima pekee.
Vijana waliotokomea vijiweni wanapaswa kunanusuliwa, watolewe huko waliko, warekebishwe tabia, wasaidie kuishi maisha bora. Haki ya kuishi maisha mazuri ni ya kila mwanadamu.
Haipendezi katika nchi hiyo hiyo wawemo wachache waliozungukwa na utajiri, huku rika la kati ambalo ni tegemeo la taifa imara likaachwa likijikuna kwa dhiki.
Ushahidi kuhusu hali za vijana wetu unajionyesha mitaani. Wapo wanaoketi chini ya miti wakipiga soga. Wengine vibarazani, maeneo ya biashara japokuwa hana afanyalo.
Wengine kwenye vibanda vya simu, vijiwe vya washona viatu, fundi saa. Wapo wenye mali za biashara, wengine hujichimbia maeneo hayo kwa shughuli tofauti kabisa kama hiyo ya kuuza kete na madawa ya kulevya na kadhalika.
Programu ziandaliwe vijana hawa wanasuliwe. Wakikalishwa chini, kila mmoja ataeleza matarajio yake.
Wizara inayoshughulikia vijana ipo. Inafanya nini juu ya kundi hili? Sera ipo? Kama haipo inasubiri nini?
Tuokoe kundi hili. Tusiwaache vijana wetu waishie kuwa machizi na mbumbumbu.
Hata nafasi za ajira zilizotangazwa kuwa zitaongezwa na serikali hazitalinufaisha kundi hilo kwa sababu wengi wao wameshakata tamaa.
Wasalaam
fwingia@yahoo.com
|