|
Mama Salma Kikwete aalikwa onyesho la wanamuziki wa kike
2006-12-25 10:19:54
By Renatha Msungu
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa albamu ya Tanzania Women All Star, uliopangwa kufanyika mwanzoni mwa Januari.
Wanamuziki hao, ambao walikutana katikati ya wiki iliyopita na CHAMUDATA, katika ukumbi wa Vijana Social, wamepania kuonyesha vitu vyao siku hiyo.
Akizungumza na Nipashe,Katibu wa Chama cha muziki wa dansi nchini CHAMUDATA, Hassan Msumari alisema uzinduzi huo utafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Aidha aliongeza kusema albamu hiyo ina jumla ya nyimbo sita.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni pamoja na Haki Sawa kwa wanawake, Vita Dhidi ya Ukimwi, Magonjwa hatari ya Kinamama, Tanzania nchi yenye Amani na Neema Tele,, Awamu ya Nne ya Kikwete na Mafanikio yake, na miaka 45, ya Uhuru.
Alisema pia bendi hiyo ina wanamuziki wa kike ambao ni nyota katika bendi zao mbali mbali.
Kwa kweli maandalizi ya albamu hiyo yanaendelea, mpaka Januari itakuwa tayari, alisema Msumari.
Alifafanua zaidi ya kuwa, lengo lao ni kuweka maandalizi mazuri kwa ajili ya sherehe hiyo.
|