|
TEFA yasalimu amri yakubali kufanya uchaguzi mwakani
2006-12-25 10:21:40
By Onesmo Kapinga
Uongozi wa Chama cha Soka wilaya ya Temeke, TEFA, chini ya mwenyekiti Thobias Otto na katibu msaidizi wake Hassan Mpanjila wamesalimu amri ya serikali ya kuzuia mkutano wao na kukubali kufanya uchaguzi Januari 13, mwakani.
Akiongea na Nipashe, jijini, Dar es Salaam, Mpanjila alisema kuwa klabu wanachama wa TEFA, juzi walitaka kufanya mkutano ulioitishwa na kamati ya utendaji wa chama hicho, lakini mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Kihato aliuzuia.
Mpanjila alisema kuwa kutokana na agizo hilo la mkuu wa wilaya, uongozi wake na klabu wanachama wa TEFA, wameheshimu maagizo yake.
Alisema kuwa mkuu huyo, amewataka wafuate maagizo ya barua ya kamati ya michezo ya mkoa Dar es Salaam, KMMD, iliyowarudisha madarakani baada ya muda wao wa uongozi kumalizika tangu Juni 21, mwaka huu.
Katika barua hiyo, TEFA, waliagizwa washirikiane na kamati ya michezo ya wilaya ya Temeke, kuandaa mkutano mkuu wa uchaguzi ndani ya siku 90, tangu waliporejeshwa madarakani.
KMMD ilipendekeza uchaguzi huo kufanyika Novemba 26, ambapo kamati ya utendaji ya TEFA, ilikubaliana na tarehe hiyo.
Hata hivyo, halmashauri kuu na mkutano mkuu wa TEFA, ulisogezwa mbele uchaguzi huo, na kupanga ungefanyika Desemba 24, kwa kutumia katiba mpya, ambayo msajili wa vyama vya michezo nchini, amesitisha kusajili marekebisho mapya ya katiba za wilaya na mkoa ikiwemo ya chama hicho.
Mpanjila alisema kuwa amekubali kuheshimu maagizo ya mkuu wa wilaya na mkutano mkuu wa viongozi wa TEFA utafanyika Januari 13.
Kamati ya michezo ya wilaya ya Temeke hivi karibuni ilitangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa TEFA baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao wa uongozi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya michezo wa wilaya ya Temeke, Shaban Mchumira Kamati ya nidhamu na usuluhisho ya wilaya hiyo, iliyokutana na uongozi wa TEFA, ulikubaliana uchaguzi ufanyike siku hiyo kwa kutumia katiba ya zamani.
Mchumira alisema kuwa katika kikao chao kiliamua Desemba 22 iwe ni siku ya kuchukua fomu kwa wagombea, Januari 2, kurudi, Januari 5, usaili kwa wagombea na Januari 13 ni siku ya uchaguzi mkuu.
|