25 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

SMZ yazindua kamati maalum ya michezo
 
2006-12-25 10:22:23
By Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, (SMZ), imeunda kamati maalum ya kitaifa ya kuchangia michezo, katika hatua za utekelezaji wa sera ya michezo Zanzibar.

Kamati hiyo ilizinduliwa mjini hapa na Naibu Waziri Kiongozi, ambaye pia ni Waziri wa Michezo, Ali Juma Shamuhuna.

Akizindua Kamati hiyo, alisema sekta ya michezo itapata mafanikio pale mchango wa jamii utakapoweza kutumika vizuri katika kuinua michezo Visiwani.

Shamuhuna alisema Zanzibar hadi sasa ina vyama vya michezo 27 na vyote vinahitaji kusaidiwa ili viweze kuwaandaa wanamichezo na viweze kushiriki mashindano mbali mbali ya kimataifa.

Alieleza kwamba sera ya michezo tayari imepitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuundwa kwa kamati hiyo ni hatua ya utekelezaji.

’’Viongozi wa kamati naomba lazima muhakikishe, vyama vitakavyonufaika ni vile vitakavyoonesha uaminifu na mikakati yake ya kuanzisha vyanzo vya mapato kabla ya kusaidiwa’’, alisema Shamuhuna.

Naibu Waziri Kiongozi alisema kwamba Tanzania ina watu wa kutosha wa kusaidia sekta ya michezo kama itakuwepo mipango mizuri na kuwatumia viongozi wa kitaifa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alitoa mfano viongozi kama vile Waziri Mkuu Edaward Lowassa, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi wana uwezo mkubwa wa kufanikisha juhudi za kuinua michezo Zanzibar, kama kamati hiyo itawatumia vizuri.

Alisema kwamba watu wenye uwezo wa kusaidia sekta ya michezo wapo wakutosha, lakini hawajahamasishwa na kuweka mazingira mazuri ya kuinua michezo.

Alieleza kwamba serikali ya Zanzibar imeamua kufufua michezo yote iliyokuwa ikifanyika siku za nyuma, kama vile mashindano ya baiskeli ngalawa na michezo mingine ambayo sasa inaonekana imedhorota.

Aidha alisema viongozi wa vyama vya michezo lazima waondoe tabia ya kulalamika pale wanapokosolewa, ili lengo la kuinua michezo lifikiwe.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ali Mzee Ali alisema kwamba kamati hiyo itaweza kufikia malengo yake iwapo wananchi watajitokeza vyakutosha kuchangia mawazo yao na fedha katika kuinua michezo Zanzibar.

Katibu wa Kamati ni Said Shaaban na inawashirikisha wafanyabiashara maarufu, akiwemo Mohammed Raza, Abdulsatar Daudi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na wenye viwanda Zanzibar, Abbas Abadalla, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Zanzibar, Sherry Khamis.

Wajumbe wengine ni Naibu Gavana wa Benki Kuu Tanzania, Juma Reli, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji katika sekta ya utalii, Zanzibar (ZATI) Simai Mohammed, Rais wa TOC, Gulam Abdalla na Mkurugenzi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar, Yussuf Omar Chunda.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.