25 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Shirikisho la A.Mashariki: Wananchi wasita viongozi wapigia debe
 
2006-12-25 11:02:25
Na Herman Kirigini

Mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi wa Afrika Mashariki juu ya kuanzishwa au kuundwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki umeazishwa rasmi katika nchi zote tatu yaani Tanzania, Kenya na Uganda.

Bila shaka madhumuni ya mchakato huu ni kukusanya maoni ya wananchi ili kuweza kupima kukubalika kwa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Ili kuwawezesha wananchi wa Afrika Mashariki kushiriki vilivyo katika mchakato huu ni jambo la lazima kwa wananchi kuwa na uelewa wa kutosha wa hali ya uchumi, kisiasa na utamaduni ya nchi zetu tatu ambazo ndizo zitakazoanzisha shirikisho la Afrika Mashariki kwa maendeleo ya eneo hili la Afrika.

Jambo lingine muhimu ni kwa mchakato huu kuwashirikisha wananchi wengi zaidi katika makundi yao yote kabisa.

Makundi hayo ni kama yale ya wanawake, vijana, wanaume, wazee, walemavu, wasomi, wanasiasa, wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi, waumini wa madhehebu ya dini, wafanyakazi na wanafunzi wa vyuo mbalimbali, n.k

Hali kadhalika lingekuwa pia jambo la maana kama mchakato huu utapewa muda wa kutosha ili ukubalike na kurahisisha ushirikishwaji na ushiriki wa wananchi.

Mijadala ya kukusanya maoni lazima iendeshwe kwa taratibu zilizo huru kabisa na za kidemokrasia.

Mambo ya uchumi ni muhimu kuzingatiwa katika mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi wa Afrika Mashariki
Uchumi wa Tanzania na Uganda unategemea zaidi kilimo cha mazao huku ule wa Kenya unategemea zaidi viwanda na huduma.

Hali hii inaufanya uchumi wa Kenya kuwa imara zaidi kushinda ule wa Tanzania na Uganda ambao unategemea hali ya hewa wakati ule wa Kenya unategemea zaidi uzalishaji wa bidhaa za viwandani.

Jambo lingine ambalo ni muhimu ni ukweli kwamba Kenya inauza bidhaa nyingi za viwandani kwa Tanzania na Uganda kuliko nchi mbili zinavyouza bidhaa hizo huko Kenya.

Kwa mfano mwaka 2005 Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya $ 593.351 millioni kwa Tanzania na Uganda wakati nchi hizi ziliuza bidhaa zenye thamani ya $186.200 Millioni kwa Kenya.

Hali hii ilisababisha nakisi ya $407.151 Millions. Mwaka huo huo Tanzania na Uganda ziliagiza kutoka Kenya bidhaa zenye thamani ya $ 638.992 Millions kwa maana hiyo nchi za Tanzania na Uganda ni soko kubwa la bidhaa za Kenya.

Kwa hiyo kuanzisha soko la pamoja na Shirikisho la Afrika Mashariki ni jambo litalaloinufaisha zaidi nchi ya Kenya kiuchumi.

Kigezo kingine muhimu kuzingatia ni ukubwa wa uchumi (au GDP) wa nchi hizi tatu. kwa mujibu wa bei rasmi za kubadilisha fedha au sarafu za nchi, uchumi wa Kenya ulikuwa na thamani ya $ 16. 11 billioni ukilinganisha na $ 12.12 billioni za Tanzania na $ 7.909 billioni za Uganda. Hii inafanya nchi hizi kutofautiana kwa nguvu za uchumi.

Kigezo kingine muhimu ni ukubwa wa bajeti za nchi hizi. Kwa mfano mnamo mwaka 2005 bajeti za nchi hizo zilikuwa kama ifuatavyo:-
Mapato Matumizi
($billioni) ($Billioni)
Kenya 3.715 3.88
Tanzania 2.235 2.669
Uganda 1.845 1.904

Hali ya uimara wa sarafu za nchi hizi tatu inaonyesha kwamba uchumi wa Tanzania na Uganda hauna nguvu za kuwezesha mauzo makubwa ya bidhaa katika nchi za nje kama ulivyouchumi wa Kenya.

Kwa maana hiyo sarafu za Tanzania na Uganda ni dhaifu. Kwa mfano mwaka 2005 sh. za Tanzania 1128 zilikuwa sawa US $. sh. za Uganda 1,780 zilikuwa sawa US $ na sh. za Kenya 75 zilikuwa sawa na US $.

Masuala ya kisiasa ya kuzingatiwa katika mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi

Kisiasa bado kuna mashaka makubwa kuhusu madhumuni na faida halisi za kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki kwa wananchi wa Kenya, Tanzania na Uganda.

Hadi Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipokufa mwaka 1977 ilikuwa dhahiri kwamba wananchi wa nchi hizi tatu walikuwa wakishirikiana zaidi na hata walifahamiana kwa karibu zaidi kuliko hali ilivyo hivi sasa.

Jumuiya hiyo ilikuwa na vyombo na taasisi zilizowashirikisha wananchi wa Afrika Mashariki. Kwa mfano walikuwa na huduma za pamoja za reli, meli, ndege na fedha.

Baada ya Jumuiya kuvunjika Tanzania na Uganda ziliambulia karibu na patupu huku Kenya ikibakia na mali nyingi za jumuiya. Matokeo yalikuwa kwamba Tanzania na Uganda zilipata hasara kubwa na Kenya ilipata faida.

Hali hii imesababisha mashaka makubwa aina ya nchi na wananchi wa Afrika Mashariki.

Bado wananchi wengi wanadhani au wanaamini uanzishwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki ni sawa na jitihada za kurejesha Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977.

Wananchi hawa waliumwa na nyoka na sasa wanaogopa hata wanapoiona kamba. Ni vigumu sana kwa wananchi wa Tanzania na Uganda kuwa na imani kwamba Shirikisho litawaletea faida ambayo inaweza kufidia hasara kubwa waliyoipata baada ya jumuiya ya zamani kuvunjika.

Jambo moja linalojitokeza kwa dhahiri ni kwamba kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki ni Mission inayopigiwa debe zaidi na viongozi wa kisiasa wa ngazi za kitaifa nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Pamoja na mashaka ya wananchi walio wengi bado inashangaza kuona kwamba ni viongozi zaidi ndio wanaosukuma na kutetea jambo hili.

Kwa maana hiyo ni dhahiri wananchi wanaburuzwa katika kuanzisha Shirikisho ambalo kwa dhahiri hawaoni faida zake.

Matokeo yanaweza kuwa kwamba Shirikisho litakaloanzishwa litakuwa la viongozi wa juu wa kisiasa zaidi kushinda kuwa la wananchi wenyewe.

Katika mchakato wa kuanzisha Customs Union kuelekea kwenye common Market na baadaye Shirikisho la Afrika Mashariki kumejitokeza masuala ambayo yameendelea kuwatia mashaka wananchi wengi wa Afrika Mashariki.

Kwanza ni udhaifu wa aliyekuwa Rais wa Tanzania katika kukubali Shirikisho huku akijua fika kwamba Tanzania ilivuna hasara kubwa kutokana na kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

Katika suala hili la ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki naamini Mh. Benjamini William Mkapa alikuwa dhaifu mno kiasi cha kushindwa kupima na kulinganisha hasara za ushirikiano uliopita na faida za ushirikiano ujao.

Ni dhahiri hakuangalia kwa makini maslahi ya Watanzania na Tanzania.

Pia lipo suala la madai kwamba Rais Yoweri K. Mseveni wa Uganda ana ajenda ya siri katika uanzishwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Madai hayo yanahusu tamaa ya utawala aliyonayo Rais huyo juu ya eneo la Maziwa Makuu ya Afrika Mashariki na Kati.

Tegemeo ni kuanzishwa kwa Empire Kubwa katika eneo hili itakayokuwa chini ya utawala wake kama Rais.

Madai kama haya yanaleta utata zaidi katika siasa za ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mwandishi Herman K.D.Kirigini ni Mbunge mstaafu
E mail:hkirigini@yahoo.com

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.