|
Bagamoyo kuandaa semina ya waamuzi mwakani
2006-12-26 08:38:09
By Margareth Malisa, PST, Pwani
Shirikisho la soka la wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani (BFA) limeandaa kozi ya waamuzi wa mchezo huo ambayo inatarajiwa kufanyika Januari 6, mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Chalinze mwishoni mwa wiki, mwenyekiti wa BFA, Juma Mpate alisema kuwa mafunzo hayo yatafanyika Bagamoyo mjini ambapo wakufunzi wa kozi hiyo watatoka katika chama cha waamuzi taifa,
Mpate alisema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwanoa wanamichezo ambao wameonyesha nia ya kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu katika kufanikisha mchezo huo ulio na wapenzi wengi nchini na duniani kwa jumla.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika Bagamoyo kwa kushirikisha zaidi ya washiriki 20 kutoka ndani ya wilaya na mkoa kwa jumla alisema Mpate.
Akizungumzia ada za ushiriki, Mpate alisema kuwa ada ni sh. 10,000, na gharama za mtihani shilingi 10,000 na kuwaomba wanamichezo zaidi kujitokeza katika kupata elimu hiyo ya uamuzi wa soka.
Kwa upande wake, mjumbe wa BFA na shirikisho la mchezo huo mkoa (COREFA), Karama Ahmed alisema kuwa mafunzo hayo yana nia ya kuongeza waamuzi hao ambao watakuwa wakitumika na BFA katika michezo mbalimbali.
Alisema kuwa wilaya hiyo ina upungufu mkubwa wa waamuzi kitu ambacho chama chake kimeliona hilo na kuamua kuanzisha mafunzo hayo kwa nia ya kuwapa mafunzo wadau wa mchezo huo.
|