|
CECAFA yapata mdhamini chalenji ya wanawake
2006-12-26 08:39:21
By Somoe Ng’itu
Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, limesema kuwa limepata mdhamini wa mashindano ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake.
Akizungumza jana na Nipashe kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye, alisema kuwa wamepanga mashindano hayo ya kwanza yafanyike Oktoba jijini Dar es Salaam.
Musonye alisema kuwa mwaka huu yalishindwa kufanyika kutokana na mazungumzo na mdhamini huyo kutofikia hatua ya mwisho lakini sasa hivi wamekubaliana.
Tunashukuru kupata mdhamini na mapema mwezi januari tutasaini mkataba na kumtangaza, alisema Musonye.
Aliongeza kuwa anazitaka nchi zote wanachama kuandaa timu za wanawake kwa ajili ya mashindano hayo yatakayoanza kufanyika kabla ya chalenji ya wanaume.
Tutafanya mashindano ya wanawake halafu tutamalizia wanaume, aliongeza.
Alisema kuwa jumla ya nchi tano tayari zimethibitisha kushiriki katika mashindano hayo na kusema kuwa bado nchi nyingine za ukanda huo zitatakiwa kuandika barua ya uthibitisho.
Musonye alizitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Tanzania Bara, Uganda, Rwanda, Zanzibar na Burundi.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila baada ya miaka miwili na yatakuwa yakichezwa katika nchi tofauti kama yanavyofanyika mashindano ya Chalenji kwa wanaume.
CECAFA ina jumla ya wanachama 11 na imekuwa ikiandaa mashindano ya vijana na timu za wakubwa kila mwaka kwa lengo la kukuza kiwango cha soka cha nchi hizi.
|