26 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Sportsnews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wachezaji wakatwe kodi - Mziray
 
2006-12-26 08:40:11
By George John

Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Syllersaid Mziray amesema wanamichezo hususani wa soka nchini wana wajibu wa kutozwa kodi kama wafanyakazi wengine kwa vile wanaingiza kipato chini ya mfumo wa kulipwa na si ridhaa kama sera ya taifa ya maendeleo ya michezo inavyosema.

Mziray, ambaye pia ni mhadhiri wa elimu ya utimamu wa mwili na michezo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada katika semina ya viongozi wa kitaifa wa michezo nchini iliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Alisema wanasoka nchini ni wa kulipwa wenye mikataba na ajira rasmi lakini hawatozwi chochote kutokana na kulindwa na sera ya michezo ya taifa inayochukulia michezo yote kama ya ridhaa.

Alisema kutokana na kivuli cha sera ya michezo kutambua michezo ya ridhaa, wachezaji wa soka wamekuwa wakiingia mikataba na vilabu vyao na kupewa baraka na Shirikisho la mchezo huo, TFF, bila kufuata mfumo rasmi wa uendeshaji wa michezo ya kulipwa.

Akatoa mfano wa mkataba wa mchezaji Athumani Idd unaoonyesha kuwa alilipwa milioni mbili wakati anajiunga Simba kwa mkataba wa miaka mitatu pamoja na mshahara wa shilingi 120,000 kila mwezi lakini hakuna anachokatwa kama kodi serikalini tofauti na nchi nyingine za Afrika na Ulaya zinazoendesha soka la kulipwa.

’’Inashangaza kuona mwalimu wa shule ya msingi anayelipwa mshahara mdogo usioendana na huduma anayotoa, anakatwa makato kibao... sera hii ya michezo inapaswa kubadilika kuendana na wakati ili kila mapato ayapatayo mchezaji yalipiwe kodi kwa mujibu wa sheria na kwa maendeleo ya taifa,’’ alisema.

’’Yanga ilipochukua ubingwa kila mchezaji alilipwa milioni 1.3 kama pongezi bila makato yoyote wakati huo ni mshahara wa mwalimu wa mwaka mzima. Ni lazima mabadiliko yafanyike,’’ alisema.

Wakichangia mada hiyo, viongozi wa vyama vya michezo nchini wamesema serikali hadi sasa haijatambua uwepo wa michezo ya kulipwa na kutoa changamoto kwa serikali kuifanyia marekebisho sera hiyo ya mwaka 1996 ili iende na wakati.

TFF imesema kuwa tanzania sasa hivi iko katika hatua ya kuingia katika soka la kulipwa na ilishaachana na soka la ridhaa.

  • SOURCE: Nipashe
TODAY
-----------------------------------------------
Editorial
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.