|
Simba waionya Yanga kumuacha Athumani Idd
2006-12-26 08:41:10
By Somoe Ng’itu
Uongozi wa klabu ya soka ya Simba umewataka wapinzani wao, Yanga kuachana na kiungo wao, Athumani Idd ili yasije kuwakuta yale yaliyotokea mwaka juzi walipokuwa wanamngangania beki, Victor Costa.
Costa mwaka juzi alidaiwa kusaini fomu za Yanga huku bado akiwa na mkataba na Simba na kukaa katika benchi la mabingwa hao walipokuwa Zanzibar kwenye mechi za sherehe ya Mapinduzi lakini walivyorejea jijini aliwakimbia na kurejea Msimbazi.
Katika kuonyesha kuwa Simba ni zaidi, viongozi waliokuwa madarakani kipindi hicho, Costa aliripoti kwenye kambi ya Simba iliyokuwa katika uwanja wa Polisi Kilwa akiwa amevaa jezi yenye jina la aliyekuwa katibu mkuu wa Yanga, Jamal Malinzi.
Akizungumza na Nipashe, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema kuwa wao wanafahamu kuwa mchezaji huyo ni mali yao kutokana na mkataba walioingia naye na pia kusaini fomu za kuchezea timu yao zilizokwenda katika shirikisho la soka barani Afrika (CAF) hivi karibuni.
Kiongozi huyo alisema kuwa wamekuwa wakiwashangaa Yanga kwa kusema huyo kiungo ni mchezaji wao huku wakifahamu fika kuwa mwaka jana wakati wanamsajili kutoka Polisi Dodoma waliweka wazi taarifa zake katika vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa kutokana na maneno ya kutamba yaliyotolewa na klabu hiyo huenda maamuzi ya kuvunja mkataba yakawa na nafasi ndogo licha ya mchezaji huyo kuandika barua ya kuomba radhi na kufanyika kwa mazungumzo.
Hata hivyo, Simba ikimruhusu mchezaji huyo kwenda Yanga, hataweza kuichezea kwenye michuano ya kimataifa na hivyo kusubiri kuanza kwa ligi ndogo ya ndani hapo mwezi Machi mwakani.
Mwaka jana klabu hizi kongwe hazikuwa na malumbano katika usajili baada ya kuwepo makubaliano ya kutochukuliana wachezaji, jambo ambalo mwaka huu limeonekana kutokuwepo.
|