26 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

SOH: Shirika la wasomi la kuinua maisha ya masikini Moro
 
2006-12-26 08:49:03
Na MORIS LYIMO

Jamii masikini vijijini na mijini hubakia kwenye umasikini kwa kutowezeshwa na kushiriki katika shughuli za maendeleo endelevu kwa kujitolea na kutumia teknolojia mbalimbali na wataalamu katika jamii husika.

Wasomi kadhaa wameona udhaifu huo na kuanzisha shirika linaloitwa Seeds of Hope (SOH) lenye makao yake mkoani Morogoro. Mwandishi MORIS LYIMO aliyetembelea shirika hilo anaelezea katika makala hii

Uanzishwaji wa Shirika hilo linalojulikana kwa maana nyingine kama Mbegu za Matumaini ni kupata suluhisho la kudumu la matatizo ya kijamii na kiuchumi ili kuendeleza majukumu yanayofanywa na serikali katika kuboresha shughuli za jamii za vijijini na mijini.

Dira ni kuona jamii hizo zinabadilika kuelekea ustawi na kupitia ushiriki wa kujitolea kutoka kwa wataalamu waliopo na pia jamii zote katika shughuli za maendeleo endelevu, kwa ajili ya kuzalisha vipato na kubuni nafasi za ajira katika nyanja za kilimo, afya, ujasiriamali, nishati na mazingira.

Mwenyekiti wa SOH Dkt.Joseph Mpagalile anasema mpango huo umekuja kuchochea ushirika shirikishi kati ya jamii za vijijini na mijini na wataalamu wa hapa nchini wenye ari katika taaluma za uhandisi, afya, nishati, biashara ya kilimo, elimu, maendeleo ya vijijini, mazingira na sheria.

Anasema mipango mingi ya maendeleo hushindwa kufanikiwa kutokana na jamii kutoshirikishwa kikamilifu katika kupanga na kubuni miradi ya maendeleo ambayo ikitekelezwa itawaondoa katika umasikini.

’’Ndiyo maana sisi tumeliona hilo na kuanzisha shirika hili baada ya kukaa na wataalamu wa mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Iringa na hapa Morogoro kuona uwezekano wa kuziondoa katika umasikini jamii masikini za mijini na vijijini kwa kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na serikali za kuwaletea wananchi maendeleo,’’anasema Dkt. Mpagalile.

Mwenyekiri huyo anasema utelelezwaji na mafanikio ya malengo yake yatafikiwa kwa kuwa na mseto wa wanachama wasomi wa juu, kati na chini, kuthamini michango yao bila kujali elimu yao, jinsia, umri, imani za kidini na hali ya maumbile yao.

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) katika ripoti yake ya mwaka huu inaonyesha kwamba, Tanzania ni ya 162 kati ya nchini 177 kwa umasikini duniani.

Hali ya umasikini nchini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita kama ilivyoonekana katika ripoti ya utafiti wa mtandao wa mashirika ya haki za binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRiNGON) ulioonyesha hali hiyo ya umasikini ilizingatia vipimo vya hali ya maendeleo ya watu vinavyoangalia umri wa kuishi, elimu na vipato halisi vya watu vilivyopimwa na shirika hilo.

Licha ya serikali kujitahidi kuweka sera, sheria na mikakati ya mipango ya maendeleo ili kupunguza umasikini nchini, bado umasikini ni tatizo kubwa hasa kwa jamii zinazoishi vijijini.

Kutokana na hali hiyo, UNDP, SAHRiNGON na wadau wengine wa maendeleo wanasisitiza kwamba kila mtu kwa nafasi yake kupambana na janga hilo kwa kadri ya uwezo wake.

Shirika la kazi Duniani (ILO) liliwahi kufanya utafiti hapa nchini na kubainisha kwamba umasikini unawafanya Watanzania wengi kuishi kwa dola moja ya kimarekani kwa siku.

Umasikini husababisha wananchi kutopata haki zao za msingi kama afya, elimu, huduma za kisheria kama mahakama, biashara isiyokuwa endelevu, uhakika wa chakula na uongozi.

Katika nchi zilizoendelea kuna chakula kingi cha kutosha na ziada ambacho kama kingetolewa ingetosha kumlisha kila mtu katika nchi masikini.

Hata hivyo Dkt.Mpagalile anasema kufanya kazi pamoja na washiriki wengine walio na mtizamo na misheni za kimaendeleo inaweza kufikia ukomo wa umasikini unaozikabili sehemu kubwa ya jamii za vijijini na sehemu chache ya watu waishio mijini.

Ushiriki huo unaweza kuzifanya jamii hizo hatimaye kuelekea kufikia ulimwengu uliostawi na endelevu pale tu wataalamu na ndani watakapoamua kujitolea nguvu za utaalamu wao katika kufanikisha mikakati inayoandaliwa kwa ajili ya kuondoa umasikini kama vile Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUKUTA).

Uendelezwaji wa elimu utakaofanywa na shirika hilo, anasema itakuwa ni kupitia uanzishwaji wa viwezesho vya elimu, kutoa vifaa vya elimu na ushiriki wa kujitolea

katika ufundishaji wa wale wasio na nafasi katika jamii.
Pia kukuza na kutumia mali asili katika ngazi ya kijiji ili kuleta maendeleo endelevu katika uhakika wa chakula na uzalishaji wa kipato, kuwezesha jamii kuwa na teknolojia na mbinu rahisi na muafaka katika maendeleo kwa kutumia wataalamu waliounda shirika hilo katika mfumo wa kujitolea kama chachu ya maendeleo.

Malengo mengine ni kuiwezesha jamii za vijijini na mijini, hasa vijana wasio na nafasi kwa kuwapa mbinu sahihi za kujikinga na Ukimwi, kuonyesha ushiriki wa wanataaluma waliopo katika jamii kuendeleza usambazaji wa teknolojia za kijamii kama namna ya kuboresha maisha ya jamii za vijijini.

Pia kuhamasisha wote kushiriki kwenye shughuli zinazolenga kulinda mazingira wakati huo huo zikizalisha kipato jamii zinazoshawishi faida za utunzaji wa mazingira.

Kuendesha mafunzo ya ujasiriamali na kuhamasisha jamii za vijijini kuwa wajasiriamali ili waweze kufaidika na shughuli kama kilimo na ufugaji, kuendesha mafunzo yasiyo ya kitaaluma katika masuala yanayoonekana kuwa na umuhimu hasa katika maeneo ya vijijini na kama itakavyohitajika na jamii husika hususan katika kuwapatia huduma kama sheria, afya, haki ya kijinsia, ardhi, demokrasia, elimu na uchaguzi.

Malengo mengine ni kuelimisha jamii namna ya kuongeza upatikanaji wa elimu kwa walio na nafasi finyu, kupunguza idadi ya watoto wanaokatisha masomo na kuchangia kufanya vizuri zaidi kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya chini.

Pia kusambaza mbinu ndogondogo, na rahisi za ubunifu za kutumiwa na watu baada ya uvunaji wa mazao zinazoweza kuongeza thamani kwenye mazao yao ya mimea na mifugo ili kuharakisha maendeleo ya jamii zinazotegemea kilimo na ufugaji.

Katibu mkuu wa shirika hilo Bw.David Msola anasema tayari shirika lao ambalo lilipata usajili Juni mwaka huu limeshajiunga na Mtandao wa vyama visivyokuwa vya kiserikali mkoani Morogoro (UNGO).

Wakati wa uzinduzi Desemba 16 mwaka huu, anasema walianza rasmi shughuli zao kwa kutembelea kituo cha watoto yatima cha Mgolole na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho.

Vitu hivyo ni pamoja na sabuni, sukari, vifaa vya michezo, mafuta ya kupikia, mchele, na maziwa maalumu ya lishe kwa watoto ambapo pia waliweza kuwafariji kwa kucheza nao.

Anasema mpango wa baadaye wa shirika lao ni kujenga shule kutoa fursa kwa watoto wasio na nafasi kuweza kusoma ikiwa watafanikiwa kupata mfadhili katika uendeshaji wa shughuli za maendeleo ya jamii kupitia shirika lao.

’’ Pia wameshaanza kutoa utaalamu wa utayarishaji wa vitalu na upandaji miti kwa vikundi mbalimbali vya kuhifadhi mazingira na uandaaji wa maandiko ya miradi.

Akizindua shirika hilo Mwenyekiti wa UNGO Bw.Modest Mkude anasema kuanzishwa kwa shirika hilo ni chachu na maendeleo kutokana na ongezeko la nguvu ya pamoja na vyama vingine vinavyounda umoja huo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.