|
Elimu yahitajika kuacha unyanyapaa kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi
2006-12-27 08:49:31
Na SHARON SAUWA
Wakati ugonjwa wa Ukimwi ukiendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu wengi, kuna umuhimu mkubwa kwa jamii kuelimishwa kuhusu kuacha tabia ya unyanyapaa kwa waathirika wa tatizo hilo.
Chumba cha mzee huyu, kiko karibu kabisa na choo ambacho hutumiwa na wapangaji mbalimbali.Hatua hiyo kwa mujibu wa maelezo ya mzee mwenyewe imefikiwa ili aweze kupata fundisho, kwa sababu hakuwa na msaada wowote wakati alipokuwa na pesa.
Hebu usituambie mambo yako hayo. Ujana wako ule raha na nani na sasa uje umtese nani. Nenda huko huko si ulikuwa na uwezo, lakini hakuna ulichotusaidia, hayo ni baadhi ya maneno ya kejeli ambayo anakumbana nao mzee mmoja (jina limehifadhiwa) katika Manispaa ya Morogoro.
Nyumba hiyo ni urithi walioupata kutoka kwa wazazi wao, ambapo watoto zaidi ya watatu wanakodolea macho.
Aliweka wazi wakati akielezea kuhusu unyanyapaa anaokumbana nao.
Hata hivyo, kinachofurahisha zaidi ni kuwepo kwa mtu mmoja katika familia yake, angalau amekuwa akimsaidia mzee huyu, ambapo kutokana na majukumu aliyonayo katika ndoa amekuwa wakati mwingine akishindwa kufanya hivyo.
Ukikitazama chumba hicho, unaweza kushuhudia ratiba maalum ambayo inaonyesha muda wa kula na kunywa dawa zake, lakini hiki kinaweza kuwa ni kitu pekee ambacho tunaweza kujifunza katika maisha ya mzee huyu, ambayo kwa kiasi kikubwa yamejaa uchungu kutokana na unyanyapaa.
Katika chumba hicho kidogo kuna meza, kabati na kitanda pamoja na radio ambayo anasema imeweza kumpatia taarifa mbalimbali toka seehemu mbalimbali za ulimwenguni wakati akiwa amelala au kujipumzisha chumbani.
Kwa sasa, mzee huyo ni mgonjwa hata kutembea ni matatizo kutokana na miguu kuvimba kwa kiasi kikubwa pamoja na uso.
Mmoja wa watu wengine ambaye amekumbana na mikasa ya kunyanyapaa ni mkazi mmoja wa Area C katika manispaa hiyo.
Hata hivyo, ameweza kuwa wazi kwa familia yake, lakini kwa majirani na watu wengine ameshindwa kufanya hivyo kwa sababu atakapofanya hivyo atakabiliana na unyanyapaa mkubwa.
Nilikuwa nikisimamia wafanyakazi katika kiwanda fulani,wakaanza kuniambia kuwa bosi vipi mbona unaopungua sana siku hizi ama miwaya nini (virusi vya Ukimwi),anafafanua jinsi alivyokuwa akifanyiwa kejeli na wafanyakazi hao wakati alipoanza kupungua uzito kwa kasi.
Mitazmo ya watu hao anasema, ilikuwa ni kweli maana hata matundu ya mikanda ya suruali yake alianza kuyapunguza ili angalau aweze kuvaa suruali.
Mwenendo wa maisha yao uliendelea kuwa hivyo hadi siku moja alipoamua kuvunja ukimya mwaka 2003 na kumshauri waende wakapime ili waweze kufahamu hali ya afya zao.
Anasema walikwenda kwenye kituo cha Angaza katika manispaa ya Morogoro na kupokea ushauri nasaha kabla ya kupima na kisha kuchukua vipimo.
Mara baada ya tukio hilo, anasema walipewa majibu ambapo akaonekana ameathirika, lakini mwenzake (mkewe) alikuwa ni mzima wa afya.
Namshukuru mke wangu alipokea majibu bila kunung\unika wala kunilaumu na akawa akinisaidia kunipeleka kwenye matibabu, sambamba na kuhakikisha kuwa anapata chakula bora, anasema Hamis ambaye mkewe ni mwalimu wa shule moja katika manispaa hiyo.
Anasema kwa kuwa mshahara wa mkewe ambaye ni mwalimu wa shule moja ya msingi katika manispaa hiyo ni mdogo, aliamua kuuza nyumba moja, ili waweze kuwasomesha watoto na fedha zitakazobakia wamalizie ujenzi wa nyumba yao.
Hivi sasa yeye ni mwanachama wa Chama cha Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi mkoani Morogoro (Wavumo), ambapo chama hicho kimekuwa faraja kubwa kwake, kwani amekuwa akikutana na watu wenye hali kama yake na hivyo kubadilishana mawazo.
Yeye ni mmoja wa watu wanaotumia dawa za kurefusha maisha,ARV ambazo anasema kwa kiasi kikubwa zinahitaji kula lishe bora, kwani kila anapozitumia njaa humshika kila mara.
Jane Macha ambaye ni Mratibu wa programu ya kupima virusi katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro, anasema unyanyapaa umekuwa ukisababisha wenye virusi vya ugonjwa huo kusafiri umbali mrefu kwa kuhofia kujulikana katika maeneo wanayoishi.
Anasema kwa mfano, wamekuwa wakipokea wagonjwa kutoka Dar es Salaam ambao wanakwenda kutafuta huduma hiyo katika hospitali hiyo.
Rehema Idd (27), anaweza kuwa miongoni mwa wanaharakati wakubwa katika mapambano ya unyanyapaa, ambapo anasema haikuwa kazi ndogo katika kuhakikisha kuwa anashinda dhamira yake.
Adha kubwa anasema alianza kuipata pindi tu alipoanza kujitokeza mbele ya kadamnasi ya watu na kuwaambia kuwa yeye anaishi na virusi na hivyo kuwahamasisha kwenda kupima ili waweze kuishi kwa matumaini.
Anasema alikumbana na unyanyapaa kwa mara ya kwanza katika familia yake ambapo walimweleza kuwa mambo ya kujitokeza hadharani ni kuidhalilisha familia yake.
Lakini sasa, anasema anafurahia na ushindi aliopata baada ya kipindi hicho kigumu katika maisha yake, kwani aliweza kuwashawishi na ndugu zake, kwenda kupima, ambapo wawili waligundulika kuwa wanaishi na virusi hivyo na sasa wote wapo katika shirika lisilo la kiserikali la Faraja.
Lakini anasema hata katika biashara zake alilazimika kubadilisha biashara na kuacha kuuza viminika (juice) na kuuza vitu vingine baada ya kugundua kuwa watu walikuwa wakikataa kununua kwa kuhofia kuambukizwa virusi.
Mwanzoni nilikuwa nikiuza juisi madumu manne ambapo nilikuwa nikipata mpaka sh 18,000 lakini ikafika wakati hata dumu moja lilikuwa ni tabu kuisha,anasema.
Anasema hata maandazi aliyokuwa akiuza kilo kati nne na tano, yalikuwa hayaishi na hivyo kumsababishia hasara kubwa.
Anasema baada ya kugundua kuwa wanakataa kununua kutokana na hofu hiyo, aliamua sasa kutengeneza karanga na kuuza sigara na kisha wakanunua cherehani.
Rehema anasema hayo yote wanayafanya katika kupambana na unyanyapaa na kuweza kumudu maisha yao ya kila siku.
Unyanyapaa umekuwa kikwazo kikubwa katika kupambana na kasi ya maambukizo ya ukimwi, imefika wakati sasa wa kuvaa silaha na kutupa pembeni lawama na badala yake kila mmoja kushughulika na tatizo.
Hapo ndipo tutakapoona mzee anaishi katika kichumba kidogo kilichopo karibu na choo akiangaliwa kwa hisia tofauti na kuacha kutupiwa vijembe visivyotia matumaini bali kumkatisha tamaa.
|