|
Uwekezaji unaoliza wananchi badala ya neema hautufai katu
2006-12-27 08:50:37
Na Mhariri
Nia ya Serikali yetu kukaribisha wawekezaji katika kuinua sekta mbalimbali nchini ni njema kabisa.
Awamu hii ya nne imejipanga vema katika kusimamia eneo hilo kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi.
Jitihada hizo zimeonyeshwa bayana na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi cha miezi sita ya mwisho iliyokamilisha mwaka mmoja wa Serikali yake kuwa madarakani Desemba 21, mwaka huu.
Katika kuhamasisha wawekezaji, alifanya ziara kadhaa muhimu nchi za nje ambapo alitembelea Marekani, China, Japan, Korea ya Kusini na pia nchi za Uarabuni.
Makusudio makubwa ya Serikali yakiwa ni kuhimiza wawekezaji waje ili uchumi wetu ukue.
Kwa hilo, hata Rais mwenyewe alisema mwelekeo ni mzuri.
Kinacholengwa hasa katika uwekezaji ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, hasa kwa kuwapatia ajira.
Watanzania walio wengi, waliamini na wanaendelea kuamini kwamba uwekezaji maana yake ni kubadili hali za maisha yao kiuchumi na siyo kuendelea kuyazorotesha.
Wawekezaji wawe msaada kwa wananchi badala ya kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa.
Kipo kilio kilichotolewa mwishoni mwa wiki na wananchi wa Kata ya Olmolog wilayani Longido, mkoani Arusha wakiomba serikali kuingilia kati na ikiwezekana kumwajibisha mwekezaji mmoja, raia wa Uingereza ambaye ameharibu ekari 340 za mazao yao mbalimbali.
Mwekezaji huyo alinyunyizia dawa ya kuulia magugu kwa kutumia ndege katika shamba lake la Mountainside, ambalo ni mali ya Kampuni ya Bia Tanzania(TBL).
Jambo hili limewakera wananchi, viongozi wa Kata hiyo pamoja na Mbunge wa Jimbo la Longido, Bw. Lekule Laizer.
Kitendo hiki, bila shaka, kimeshusha matarajio ya wananchi hao ya kupata mavuno mengi hasa baada ya mvua nzuri zinazoendelea kunyesha nchini kote.
Mashamba yaliyoharibiwa ni ya maharage, ngano na njegere, mazao ambayo ni ya chakula pia kwa ajili ya biashara.
Wawekezaji wa aina hii wasiothamini mali na jasho la wananchi, tunadhani hawatufai. Wanapaswa kuwa na nidhamu ya kujali wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji.
Hakika, wananchi walio maeneo ya uwekezaji, matarajio yao ni kunufaika na siyo maendeleo yao yazidi kuzorota.
Mwekezaji yule alipaswa kuweka tahadhari kama ambavyo aliwahi kushauriwa na wataalamu wa kilimo kwamba asitumie ndege kwa sababu hewa itasambaa katika mashamba mengine na badala yake atumie trekta kupulizia, jambo ambalo alipuuza.
Serikali pamoja na nia nzuri ya kukaribisha uwekezaji, ni muhimu pia kufuatilia watu hawa kwani inaonekana wapo wenye viburi na wasiojali masharti ya uwekezaji, hivyo kujifanyia mambo watakavyo.
Matokeo yake ndio kama yaliyowakumba wananchi wa Longido ambao furaha ya kuvuna mavuno mengi imefifia ghafla.
|