31 Dec 2006 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Tujiulize tumefanya nini 2006
 
2006-12-31 09:25:06
Na Mhariri

Leo ni siku ya mwisho katika mwaka huu wa 2006.
Itakapofika saa sita na dakika moja usiku wa leo, tutakuwa tumeanza siku nyingine, mwezi mwingine na Mwaka Mpya wa 2007.

Kwa mantiki hiyo tunatarajia kuona furaha za wengi usiku wa leo kwa kufanikiwa kuuona Mwaka Mpya, hasa kwa kuzingatia kwamba tunao wengi ambao Mwenyezi Mungu, amewaita kabla ya kuuona mwaka mpya.

Wakati tunasherehekea Mwaka Mpya kesho, kila mmoja wetu anayo mengi ya kujiuliza.

Amefanya nini katika ustawi wa maisha yake katika kipindi chote cha mwaka unaoisha leo na ana matarajio gani katika mwaka unaoanza kesho.

Tunajua wengi wetu tunaendesha maisha yetu bila malengo ama matarajio, lakini pengine ni wakati mwafaka sasa wa kila mmoja wetu kujiwekea malengo fulani, ambayo mwisho wa mwaka unaoanza kesho, atakuwa na kazi ya kujiuliza kama ameyafikia ili apime ni wapi alipokwama na kwa nini.

Wakati kila mmoja wetu anayo mambo ya kujiuliza na kujipangia yale anayotarajia kuyafikia katika kipindi cha mwaka unaoanza kesho, sisi kama taifa tunayo mengi ya kujiuliza pia, hasa kwa kuzingatia kwamba ndio kwanza tumemaliza mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Hii ni serikali tulioichagua sisi wenyewe kwa kura nyingi, kila mmoja wetu akitarajia kwamba itatufikisha kwenye Tanzania Yenye Neema Tele.

Tunakubaliana na usemi kwamba kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza ameifanyia nini Tanzania katika mwaka huu unaoisha, lakini bila shaka anayo haki pia ya kuuliza serikali aliyoichagua, imemfanyia nini ama ina uelekeo upi katika kumwekea misingi yenye maisha bora.

Tumaini kubwa la Watanzania katika Serikali ya Awamu ya Nne ni kuwaondolea umaskini.

Hata serikali hiyo kupitia kwa Waziri Mkuu na Rais mwenyewe, wameeleza katika hotuba zao wakati wanamaliza mwaka mmoja wakiwa madarakani. kwamba wako kwenye msitari na wanaridhika na mwenendo wao.

Je, sisi wananchi tunapojiuliza maswali tunaona ni kweli viongozi wako kwenye msitari na mwaka ujao tutapiga hatua kubwa zaidi katika kumfanya kila Mtanzania awe na Maisha Bora kama walivyokuwa wakituambia wakati wanatuomba kura?

Misingi ya kuandaa maisha bora kwa kila mtanzania inahusisha mambo mengi.

Baadhi ya mambo hayo ni kuimarisha miundo mbinu, na hapa tunazungumzia barabara, maji, umeme, afya, elimu na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Mwaka ulioisha tumeshuhudia tatizo kubwa la upungufu wa umeme, ambao watalaamu wanaamini kwamba ni kiungo muhimu kabisa katika kuinua uchumi wa taifa lolote lile.

Kwa bahati tunamaliza mwaka kwa kusikia kwamba mgao wa umeme umekwisha baada ya mabwawa kujaa maji, huku viongozi wetu wakiahidi kwamba wamechukua hatua nyingi, kuhakikisha kwamba mwaka ujao na kuendelea, hatukumbwi tena na tatizo la mgao wa umeme.

Kinachotutia wasiwasi ni kama kauli hizi ni za kweli ama ni za kisiasa. Wakati serikali inatiliana mkataba na IPTL, tuliambiwa kuwa sasa mgao wa umeme, itakuwa hadithi, lakini sisi wenyewe tumeshuhudia tulichoshuhudia.

Baadaye serikali ilitiliana mkataba na SONGAS tukaambiwa kuwa mgao wa umeme ungekuwa hadithi, lakini tumejionea wenyewe.

Hata wakati mgao huu unaanza mapema mwaka huu, tulikuwa tunapewa ahadi hizi na zile, kwamba mgao utaisha ifikapo mwezi ujao, lakini wapi!

Hatujakusudia kulaumu serikali kwa kauli hizi tata, lakini tunataka ijitahidi kutimiza ahadi zake, ili wananchi wawe na imani nayo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.