|
Mkeo yuko ubavuni, lakini wewe busy wamtomasa wa mwenzako
2006-12-31 09:27:20
Na Anti Flora Wingia
Matendo ya mtu mara nyingi hudhihirisha pia tabia yake ilivyo. Urafiki waweza kujengwa kwa muda mrefu, lakini ukavunjika kwa siku moja. na hali huchangiwa sana na ukosefu wa uaminifu.
hebu mpenzi msomaji kabla hatujaendele nikumegee kituko kimoja kilichotokea hivi majuzi mara tu baada ya sikukuu ya Krismasi.
Wajua tena wakati wa sikukuu, marafiki huketi pamoja kwa maakuli na vinywaji kusherehekea.
Lakini katika vikao hivi vya kufurahia, vituko havikosekani hasa baada ya kilevi kupanda kichwani. Adabu na heshima, ustaarabu na kadhalika hutoweka zake.
Zipo familia mbili zilizokuwa zinaheshimiana sana. wote kwa muda mrefu wamekuwa wakitembeleana kwa raha na shida.
Lakini urafiki huu uliojengeka kwa muda mrefu, uliisha kwa siku moja, kila mmoja akamuona mwenzake kama kituo cha polisi.
Ilikuwaje? Familia hizi, kila moja ikiwa ni mtu na mkewe zilialikana kutoka outing kusherehekea Krismasi.
Wakachagua sehemu nzuri ya burudani inayopendwa na watu wengi. Meza ikapatikana kisha wakaketi na kuagiza vinywaji.
Pia maakuli kulingana na chaguo la mtu. Wakati wote ilikuwa ni vicheko wakikumbushana mambo mbalimbali.
lakini, kama anavyonisimulia mmoja wa wanafamilia hao, mkao katika meza ile ulikuwa na muskeli. Bwana mmoja wapo akaketi ubavuni kabisa mwa mke wa rafiki yake.
Tena wakati wote wakiangua vicheko, bwana huyu badala ya kumshika mkewe, akawa anamshika mke wa rafiki yake iwe ni begani na wakati mwingine sehemu za mapajana.
Hiyo haikusumbua sana kutokana na imani kuwa ilikuwa ni katika kufurahia sikukuu na kwamba hakuna ubaya kwani ni watu wasiotiliana shaka kwa muda mrefu. Lakini kumbe ibilisi wa mtu ni mtu.
Ulifikia wakati bwana yule sasa badala ya kumgeukia mkewe upande wa kulia kwake, akawa anamgeukia mke wa rafiki yake kushoto kwake na kuanza kumshika sehemu za mgongoni huku mkono ukishuka hadi kiunoni.
Mwenye mke, inasemekana mara kadhaa alikuwa akiuondoa mkono wa bwana yule akifikiri ni utani.
Kumbe jamaa linafanya kweli. Sasa likaanza kupapasa utunda(shanga) za bibie. Mwenye mali kuona vile akaja juu. Ilikuwa ni kitimtimu na mfarakano ukaanzia pale pale.
Inavosemekana, ilibidi yule mwenye mke aliyekuwa akitomaswa aitishe kikao cha wanandugu kujadili tukio lile.
Bibie alijitetea kuwa japokuwa alikuwa hataki atomaswe, lakini jamaa lilikuwa linangangania tu. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.
Mpenzi msomaji, hayo ndio mambo ya marafiki. Urafiki wa mashaka hata ufanyeje siku moja utadhihirika tu. Kituko hiki kimenikumbusha maneno niliyowahi kusoma katika kitabu cha Biblia Takatifu kuhusu URAFIKI.
Ndani yake nikajifunza kwamba ukitaka rafiki, mpime kwanza, usiharakishe kumwamini kwani kuna rafiki aliye rafiki inapofaa, siku ya taabu hayuko nawe kukusaidia.
Pia kuna rafiki ageukaye kuwa adui kwa kuzusha ugomvi ili kukuabisha. (kama jamaa aliyezua kituko kwa kudodosa mke wa rafikie).
Na yuko rafiki ambaye ni rafiki wakati wa mlo, lakini siku ya tabu anakaa chonjo.
Mbali na hayo, usisahau kwamba rafiki mwaminifu ni kinga imara. Ukibahatika kumpata rafiki wa aina hii, basi ujue umepata hazina.
Rafiki mwaminifu ana thamani kuliko chochote...hakuna awezaye kupima ubora wake. Mtu mwaminifu ni dawa itiayo nguvu mwilini.
Na wale wote wamchao MUNGU ndio wanaompata rafiki wa aina hii. Hupata marafiki wa kweli kwa maana, alivyo mtu, ndivyo walivyo na marafiki zake.
Mpenzi msomaji, Kituko nilichogusia kimejikita sana ndani ya jamii yetu. Na hiyo ni kutokana na ukweli kwamba uaminifu umewekwa kando, hivyo watu kuchuma dhambi hadharani.
Vituko vya aina hii mara nyingi huibuka ulevini. Watu wanapobugia machicha huwa na tabia ya kujisahau na kuvunja uaminifu ambao nao huvunja urafiki.
Utaona mtu amemtoa outing mpenzi wake au mke na mume wamejisikia kuwa nje ya nyumbani mahali pa burudani. Pale kila mtu hufika kujiliwaza kwa dansi na vinywaji.
Baada ya kuchangamka, baadhi ya watu wana tabia ya kujisahau kama yuko na mpenziwe na hivyo kuanza kupepesa macho.
Kama rhumba linasakatwa ukumbini, basi watu wengine macho huwatoka pima kuangalia nani ananengua vema. Akishamnasa mmoja, basi anakufa naye. Bila aibu atamuomba mkewe au mumewe ruhusa akacheze na fulani, eti ni Jealous time.
Akimruhusu linakuwa ni kosa. Manake hiyo mikumbatiano siyo ya kawaida. Sasa mama aliyebakia kitini kwanini asilie wivu?
Wapo watu wameachana kwa vituko vya aina hii. Na yote hayo ni kutokana na watu kutamani vya wenzao japokuwa chake anacho, tena ubavuni mwake. Maisha Ndivyo Yalivyo.
Wasalaam
Email:f wingia@yahoo.com
|