03 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Serikali iajiri walimu bora na si bora walimu kukabili upungufu
 
2007-01-03 08:49:03
Na HAROLD JOHN

Hatua za dharura zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabili upungufu mkubwa wa walimu katika shule za sekondari, ni muhimu sana ukazingatia ubora wa walimu watakaokabidhiwa dhamana ya kufundisha wanafunzi na elimu itakayotolewa shuleni kama tunataka kuona taifa linapiga hatua kielimu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bibi Margareth Sitta wakati akilihutubia Bunge mwaka jana, alisema kuwa, ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) umeleta mafanikio makubwa ya kuinua kiwango cha elimu ikiwa ni pamoja na kutoa fursa nyingi zaidi kwa wanafunzi kwenda shule na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Hata hivyo, wakati mafanikio hayo yakiendelea kupatikana kwa wanafunzi kufanya vizuri na kushinda mitihani yao, kumeibuka tatizo jingine la uhaba mkubwa wa walimu katika historia ya nchi yetu.

Hadi kufikia wakati akitoa taarifa hiyo Bungeni, ni kwamba kulikuwa na mahitaji ya walimu wapatao 9,500 wanaohitajika katika shule mbalimbali za sekondari kwa mwaka ulioisha hivi karibuni, ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya SEDP kufanikiwa kwa asilimia 49.3 ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa katika kipindi hicho cha asilimia 40.

Kimsingi alisema kuwa, asilimia 49.3 iliyofikiwa ilikuwa imelengwa kufikiwa katika kipindi cha mwaka 2009 na kwamba suala hilo ni la kujivunia kwa kupatikana mafanikio hayo.

Miongoni mwa hatua ambazo kwa mujibu wa Waziri Sitta zilikusudiwa kuchukuliwa ili kukabili uhaba huo wa walimu ni kuajiri walimu wapatao 3,207 wahitimu wa ngazi ya Diploma toka katika vyuo mbalimbali vya ualimu wakiwemo walimu 500 ambao wamehitimu katika vyuo vikuu.

Hata hivyo alisema, pamoja na hatua hizo kuchukuliwa kama zitafanikiwa kikamilifu,bado kutakuwa na mahitaji ya walimu wapatao 5,793.

Aliliambia Bunge kuwa, mpango mwingine ni kuajiri walimu wastaafu wapatao 250 ambao bado wana uwezo wa kufundisha ikiwa pamoja na kuajiri watu 260 wenye shahada mbalimbali walioonyesha nia ya kukabiliana na tatizo hilo.

Kama hiyo haitoshi, serikali pia iliandaa utaratibu wa kutoa mafunzo ya mwezi mmoja kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na kupata alama za daraja la tatu na kuendelea.

Alisema mpango huo kwa kiasi kikubwa utachangia katika kukabili uhaba wa walimu wanaohitajika.

Mpango huo umetengewa kiasi cha sh bilioni 8 hadi kukamilika kwa hatua hizo za dharura.

Kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu Edward Lowassa akigusia hatua za kukabili tatizo hilo hivi karibuni, alisema kuwa serikali imeandaa mpango wa dharura wa kupata walimu wengi kwa sasa ili kukabiliana na upungufu uliopo uliosababishwa na mwamko mkubwa wa kuendeleza elimu nchini.

Ufafanuzi huo, aliutoa wakati akizungumza katika harambee iliyochangisha jumla ya Sh. Milioni 61 za ujenzi wa bweni la shule ya sekondari iitwayo Irkisongo mjini Monduli, mkoani Arusha.

Mpango huo kwa mujibu wa Bw Lowassa utagharimu mabilioni ya fedha, ambayo hakuyataja kitakwimu.

Alisema uamuzi huo wa serikali umelengwa kutekelezwa kwa gharama yo yote ile, kwa vile hakuna mbadala wa elimu.

Utekelezaji wa mipango ya MMEM, MMES na wananchi kuchangia katika ujenzi wa madarasa ya shule mbalimbali imechangia kuwe na mahitaji makubwa ya walimu wa kukidhi mahitaji.

Tayari serikali imeanzisha vyuo vikuu viwili kwa ajili ya walimu. Vyuo hivyo ni Chang\'ombe cha jijini Dar es Salaam kilichobadilishwa kutoka Chuo cha Ualimu na Mkwawa mkoani Iringa iliyokuwa sekondari ya juu.

Wakati hatua hizo zinachukuliwa ni muhimu sana kwa serikali na jamii nzima kuwa makini katika hatua hizi za zimamoto ili kupata walimu wa kujaza mahitaji yaliyojitokeza.

Watoto wanahitaji elimu bora na si bora elimu katika zama hizi za ushindani na utandawazi.Yawezekana kabisa kupata idadi kubwa ya walimu,lakini je walimu hao ni bora?

Kinachotakiwa si wingi wa walimu.Wingi wa walimu bila ya ubora,yawezekana tukajikuta tunakidhi kufikia idadi kubwa ya walimu ambao badala ya kuwarithisha urithi mzuri wa elimu, wakajikuta wanavurugwa na kushindwa kumudu kasi ya mahitaji ya kielimu vya zama hizi.

Kwa hiyo, kusoma takwimu ya mafanikio ya kuwa na idadi ya walimu wanaoendelea kupatikana na kuiridhisha jamii kuwa mambo yanakwenda vizuri bila ya kuangalia ubora wa walimu hao, tunaweza kujikuta tuna idadi kubwa ya wanafunzi darasani, lakini maandalizi yao yakawa hafifu kuliko wakati wowote ule katika historia ya nchi yetu.

Kwa namna yoyote ile, walimu kuandaliwa kwa kipindi cha mwezi mmoja ni dhahiri wanakosa mambo mengi ya msingi ambayo ni muhimu katika kumjenga mwalimu amudu sio tu kufundisha wanafunzi ni pamoja na saikolojia ya ualimu.

Mwalimu anatakiwa awe na mbinu mbalimbali za ushawishi katika kumfanya mwanafunzi apende somo au masomo fulani na kumjengea mazingira mazuri ya kumfanya afanye vizuri.

Kwa sababu upo ushahidi wa kutosha kuwa mwalimu asiye na nidhamu ambaye ana uelewa mdogo wa ufundishaji huwakatisha tamaa wanafunzi, hata kuwafanya wapende kufanya mambo mengine ambayo yanaweza kuwapoteza na kuwafanya wasiwe na manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla huko mbele ya safari.

Baadhi ya walimu wasio waadilifu hutumia lugha ya kihuni ambayo wakati mwingine huwa na athari ya moja kwa moja kwa wanafunzi au kusababisha wanafunzi kujifunza mambo yasiyofaa kwa sababu wanafunzi wanawaamini walimu wao.

Kuna suala jingine ambalo linaendelea kuitafuna jamii yetu ni suala la mimba kwa wanafunzi.

Baadhi ya walimu ambao hawakuandaliwa vizuri ipasavyo,ni rahisi sana kutumia mwanya huo wa kukabidhiwa wanafunzi wawafundishe hasa wa kike,kujenga nao urafiki wa kimapenzi na kuwasababishia kupata mimba au Ukimwi.

Hali hii inaweza kufananishwa na kumkabidhi fisi zizi la mbuzi.

Idadi ya wanafunzi wa kike wanaoshindwa kumaliza shule kwa sababu ya mimba na utoro ni kubwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Jambo jingine muhimu kuhusu hatua hizi za dharura ni kufanya tathmini ya kina ili kujua ni walimu wanafunzi wangapi ambao walipewa mafunzo ya mwezi mmoja mwaka jana ambao wameripoti katika shule mbalimbali walizopangiwa na wanaendelea kufundisha hadi sasa.

Hali hii itatoa picha halisi ya ukubwa wa tatizo hilo kwa takwimu, badala ya kuendelea kuwa na idadi kubwa ya walimu wanaopelekwa mashuleni kumbe idadi ya walimu walioko huko ni ndogo sana.

Ni vyema viongozi wakuu wa serikali na wanasiasa kwa ujumla wanapozungumzia hatua za maandalizi ya walimu ili kukabili uhaba huo wakawa makini kwa hilo.

Kwa hiyo, nia nzuri ya kuandaa na kuwa na walimu wengi zaidi ili kukabili mahitaji ni ya kuungwa mkono na mtu yoyote yule mwenye nia ya kuona taifa linapiga hatua kielimu.Hii ni kutokana na ukweli kuwa elimu ni hazina nzuri katika maisha ya watu wa zama hizi.

Hata hivyo, kunahitajika kuchukuliwa tahadhari za hali ya juu ili kuhakikisha kuwa walimu wanaoajiriwa na kukabidhiwa dhamana ya kufundisha wanakuwa na ubora unaotakiwa ambao utasaidia kulisukuma mbele taifa kielimu, badala ya kuliangamiza na kurirudisha nyuma.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.