|
Ni habari njema kwa walioomba mikopo fedha za Kikwete
2007-01-03 08:50:09
Na Mhariri
Shilingi bilioni moja zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa kila mkoa, sasa zimeiva.
Serikali imetangaza habari njema kwamba wananchi wote walioandika michanganuo kuomba mikopo, waanze kupeleka maombi kwenye benki za CRDB na NMB.
Fedha hizi zilitolewa na Rais mahususi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Habari juu ya kuiva kwa mikopo hiyo, zilitolewa Jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kepteni(mstaafu), John Chiligati.
Waziri akasema kuwa, wale wote walioandika michanganuo ya miradi na kuipitishia kwenye kamati za vijiji, Kata na Wilaya, sasa wanaweza kuomba na kupewa fedha hizo.
“Serikali ilishatoa bil.10.5 kwa benki hizo tangu mwaka jana, ili zitumike kama dhamana ya kuwakopesha wafanyabiashara hao wadogo kwa wakati”, alisema Kepteni mstaafu Chiligati.
Habari kuhusu kuanza kutolewa kwa fedha hizo, bila shaka, zimewapa wananchi matumaini hasa kwa kuzingatia kwamba ni ahadi aliyoitoa Rais Kikwete, mara tu baada ya kuingia madarakani mwanzoni mwa mwaka jana.
Kwanza tunafarijika kwamba serikali yetu ya Awamu ya Nne, haina masihara katika mchakato wa kutekeleza ahadi zake, tena kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya.
Hii ni moja ya ahadi zilizotolewa na kuanza kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja. Ama kwa hakika, ni dalili nzuri kwamba serikali hii ni ya vitendo na si maneno yanayoishia makabatini.
Pili, ili lengo la serikali litimie na lizae matunda, fedha hizo ni muhimu zitolewe katika utaratibu mzuri, usio na ujanja na ziwafikie walengwa bila usumbufu.
Tunasema hivi kwa sababu uzoefu unatuonyesha kuwa huko nyuma, fedha zinapotolewa na serikali kwa ajili ya mikopo, zinaishia mikononi mwa wachache wenye nafasi na uwezo badala ya wahitaji.
Itakumbukwa upo wakati Fulani, katika moja ya awamu mbili za serikali zilizopita, zilitolewa zaidi ya mil.300 kwa ajili ya kukopesha wanawake.
Fedha hizo zilizua malalamiko mengi, huku walengwa wakipewa masharti magumu, wengine wakishindwa kuandika michanganuo ya miradi na kadhalika.
Matokeo yake wajanja wachache ndio walionufaika na kufanya zoezi zima kutokuwa na manufaa yoyote.
Haitarajiwi na hizi za Rais Kikwete zitafanyiwa upuuzi huo.
Ingawa, katika moja ya maswali aliyoulizwa Rais hivi karibuni kuhusu fedha hizo bil.10.5, aliwaondolea hofu wananchi kuwa taratibu zitasimamiwa ipasavyo.
Akasisitiza kuwa “taratibu za mikopo tumezitengeneza vizuri”.
Ni matumaini yetu kwamba, wale wote walioomba mikopo hii watatendewa haki kwa kutimiziwa maombi yao bila usumbufu.
Wakati huo huo, baada ya kuipata, tunaamini walengwa wataitumia vilivyo kwa miradi waliyokusudia na siyo vinginevyo.
Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, lengo la serikali la kuwapatia wananchi mikopo ni ili kujinasua kutoka katika umasikini kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
|