|
Celtel yabadilisha namba kuona salio, kuongeza vocha
2007-01-03 08:52:09
Na Erick Lema
Kampuni ya simu ya Celtel, imetangaza mabadiliko ya namba pamoja na huduma zake mbalimbali zikiwemo za kuangalia salio na kuongeza muda wa maongezi na kusikiliza ujumbe wa sauti.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Masoko Bi.Magreth Kositany, ilisema huduma hiyo itaanza rasmi leo kwa wateja wote wa Celtel.
Bi.Kositany alisema kupitia taarifa yake kuwa kuanzia leo huduma ya kuangalia salio kwa njia ya ussd (sms), mteja anatakiwa kupiga nyota kisha namba 102 ikifuatiwa na alama ya reli (*102#), badala ya ile ya awali ambayo ilikuwa nyota (*137#).
Alisema kwa sasa mteja anapaswa kupiga namba 102, badala ya 133 iliyokuwa ikitumika awali.
“Kuongeza salio kwa kutumia vocha wateja wanapaswa kutumia alama ya nyota halafu namba 104 halafu na nyota, ikifuatiwa na tarakimu 14 zilizofichwa,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilisema namba hizo mpya zitatumika hata kwenye vocha za muda wa maongezi.
Pia ilisema kwa huduma ya kusikiliza ujumbe, wateja wanapaswa kupiga namba 123 badala ya 120.
Ilieleza kuwa mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa muongozo na maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Mawasiliano nchini (TCRA), kuhusu mabadiliko ya namba za watumiaji wote wa simu za mkononi.
Mkurugenzi huyo aliwahakikishia wateja wa Celtel kuwa maandalizi yote yameshakamilika, hivyo wateja wasiwe na wasiwasi kwani namba hizo mpya zimeshajaribiwa na zinafanya kazi vizuri.
|