|
Bendera: Viongozi Babati acheni urasimu
2007-01-03 08:53:18
Na Thobias Mwanakatwe, PST Babati
Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wameonywa kuacha urasimu wa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Viongozi hao wameambiwa kuwa, urasimu katika utoaji wa habari, kutajenga chuki na kusababisha vyombo vya habari kuandika habari ambazo hazitasaidia kuleta maendeleo ya wilaya hiyo.
Onyo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo, Bw. Joel Bendera.
Bw Bendera alitoa onyo hilo juzi baada ya kuelezwa na waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara kuwa, wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na viongozi wa halmashuari za wilaya kutotoa ushirikiano kwao.
Kaimu Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara (MAMEC) Bw. Mohamed Simbulla katika risala alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Bw. Mashe Mbejo pamoja na Mbunge wa Babati Vijijini, Bw. Damashi Knakey, wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa waandishi ambapo pia huwanyanyasa na kuwadharau.
Kufuatia hali hiyo, Bw. Bendera alisema serikali haitawavumilia watendaji wa serikali ambao wenye urasimu wa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari hasa wanapofuatwa kwa kuwa urasimu huo unapofanyika wananchi ndio wanaoathirika kwa kukosa kupata habari.
“Sera ya habari imebainisha wazi kuwa, lazima wananchi wapate habari…mimi nawashangaa baadhi ya viongozi wanawaogopa waandishi wa habari…jamani hawa watu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, naomba tuwatumie,” alisema Bw Bendera.
Aliongeza kuwa, hata Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwasisitiza viongozi watoe ushirikiano kwa waandishi wa habari.
Alisema viongozi wa serikali lazima watambue kuwa, dunia ya leo imebakia kama kijiji kwa hiyo hakuna sababu kwa watendaji wa serikali kuficha habari kwani hata kama wakifanya hivyo kama kuna mambo ya siri yasiyofaa wanayoyafanya ambayo wanakataa yasifichuliwe na vyombo vya yatajulikana tu kwa njia nyingine.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo aliwataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi zao kwa kuhakikisha wanaandika habari ambazo ni za kweli kwani kufanya hivyo kutawajengea umaarufu na pia kutawafanya viongozi kujenga uaminifu kwao na hivyo kuwa wazi katika kutoa taarifa.
Alisema hivi sasa serikali inaandaa utaratibu wa kuwasomesha waandishi wa habari wa vyomnbo vya serikali na vile vya binafsi ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa utaalamu zaidi badala ya hivi sasa ambapo baadhi yao wanafanya kazi hiyo bila kuisomea.
“Tunaandaa utaratibu wa kuwasomesha waandishi wa habari,tunataka tuwe na waandishi wasomi siyo `makanjanja’ hawa makanjanja ndio hasa wanaoharibu sifa ya waandishi wa habari,” alisema.
Kuhusu maslahi ya waandishi,alisema serikali inatambua kuwa wengi wanafanyakazi katika mazingira magumu kutokana na kukosa vitendea kazi na kulipwa maslahi kidogo na wamiliki wa vyombo vya habari ukilinganisha na kazi wanazofanya.
Alisema suala hilo linaangaliwa na serikali namna ya kuboresha maslahi hayo.
|