|
Mtumishi wa kituo cha mafuta agongwa, afa papo hapo
2007-01-03 08:54:43
Na Raymond Kaminyoge
Mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha Engen kilichopo Mbezi, Jijini Dar es Salaam, Hamis Bontogwa (26) amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Bw. Jamal Rwambow alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea juzi saa 12:30 jioni katika barabara ya Bagamoyo eneo la Makonde Mbezi.
Alisema gari lililomgonga ni aina ya Toyota Coaster, lenye namba za usajili T464 ACQ ambalo lilikuwa likitokea Tegeta kwenda Mwenge.
Kamanda Rwambow alisema dereva huyo aliacha barabara na kuendesha pembeni mwa waendao kwa miguu kwa mwendo wa kasi ndipo alipomgonga mtu huyo.
Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva na anashikiliwa na polisi wakati mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio lingine, polisi imewatia mbaroni watu wanane wakazi wa Jangwani, wakiwa na kete 143 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Bw. Masindoki Masindoki alisema watu hao walikamatwa juzi saa 12:47 jioni katika maeneo ya Jangwani.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hussein Uledi (30), Said Issa (20), Smart Ngasa (27), George Antipas (28) na Kambi Muhidini (37).
Wengine ni Hamza Mfaume (21), Seif Abdallah (24) na Shaaban Ayoub (33).
|