03 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kiwanda cha magodoro wagoma
 
2007-01-03 08:55:39
Na Richard Makore

Zaidi ya wafanyakazi 100 wa Kiwanda cha Kutengeneza Magodoro (QFL) cha Jijini Dar es Salaam, jana waligoma kwa muda kuingia kazini wakidai nyongeza za mishahara.

Kadhalika, wafanyakazi hao walikuwa wakidai kupatiwa barua mpya za ajira zinazofafanua malipo na posho wanayostahili kupewa na mwajiri wao.

Kwa sasa wafanyakazi hao wengi wao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18, wanalipwa mshahara wa Sh. 55,000 kwa mwezi.

Wakizungumza na Nipashe kiwandani hapo jana, baadhi ya wafanyakazi ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema stahili nyingine wanazotaka kupewa ni pamoja na posho za usafiri, fedha za likizo, matibabu, nyumba na malipo ya ziada baada ya saa za kazi.

Aidha, walisema wanataka uongozi wa kiwanda kuweka bayana muda wa kumaliza kazi badala ya sasa ambapo wanajua muda wa kuingia tu kazini lakini wa kutoka haujulikani.

Walisema huingia kazini saa 2:00 asubuhi lakini siku nyingine hufanya kazi hadi saa 4: 00 usiku bila ya malipo ya ziada.

Waliongeza kuwa, licha ya kufanya kazi kwa kulipwa mshahara mdogo kwa muda mrefu, lakini pia hawana vifaa maalum vya kujikinga na vumbi jingi eneo lao la kazi.

Wafanyakazi hao walisema mara nyingi wanapouliza uongozi wa kiwanda hicho juu ya upungufu huo, hujibiwa kuwa anayetaka kazi afanye na anayehoji aache kazi.

Wakizungumza kwa kupokezana, wafanyakazi hao walidai kuwa, mauzo ya magoro yameongezeka lakini uongozi wa kiwanda hautaki kuwaongezea mishahara na marupurupu mengine kwa muda mrefu.

“Sisi ndiyo wazalishaji wakuu na tunajua mauzo yameongezeka, uongozi wa kiwanda hautaki kutuongezea mishahara ili tufanye kazi kwa moyo wa kujituma zaidi,” walilalamika.

Mgomo huo ulianza mapema jana asubuhi ambapo wafanyakazi wote walifika na kukaa kwenye lango kuu la kuingilia badala ya kuingia ndani na kuendelea na kazi.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya uongozi wa kiwanda kupata taarifa za kuwepo kwa mgomo huo, uliwaita na kuzungumza na wafanyakazi hao.

Wakizungumza na Nipashe baada ya kumalizika kwa mkutano na uongozi wa kiwanda, walisema wamekubaliana kutatua matatizo hayo mapema mwezi ujao.

Walisema Mkurugenzi wao, Bw. Hassan Ali Walii, amekubali kuwaongezea mishahara na madai yao mengine bila masharti yoyote.

Alipotakiwa kuzungumzia mgomo huo, Bw. Walii alikataa kusema chochote na kuanza kumfokea mwandishi.

“Ondoka, nenda kwanza nani kakuruhusu kuingia humu ndani? Na nyie walinzi, nani kawaambia mmruhusu aingie ndani mtu huyu?,” Alifoka kwa jazba.

Alimwambia mwandishi kama amepata taarifa za kuwepo mgomo kupitia kwa wafanyakazi basi ni bora aende aongee nao wenyewe.

Mpaka Nipashe linaondoka eneo la tukio saa 4:30 asubuhi jana wafanyakazi wote walikuwa wamesitisha mgomo na kuingia kazini.

Hata hivyo, wafanyakazi hao walidai hiyo sio mara ya kwanza kwa uongozi wa kiwanda hicho kutoa ahadi kama hiyo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.