|
Bunduki 51, mabomu, risasi 91 vyakamatwa...
2007-01-03 08:56:33
Na Stephen Wang`anyi, PST Shinyanga
Jumla ya bunduki 51 za aina mbalimbali, risasi 93 na mabomu mawili ya kutupwa kwa mikono, vimekamatwa katika operesheni maalum ya kusaka silaha na majambazi iliyofanyika mkoani humu.
Operesheni hiyo ilifanyika kati ya Desemba 16 na 30, mwaka jana.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Bw. Sirro alisema kati ya bunduki zilizokamatwa, 22 ni aina ya gobore na moja ni ya kivita ijulikanayo kama FN yenye namba 78185241 iliyokuwa na risasi 27 za bunduki aina ya SMG.
Alisema silaha hizo na mabomu zinahisiwa kutumika katika matukio mbalimbali ya ujambazi na utekaji katika Wilaya ya Bukombe na Kahama mkoani humu.
Aliwataja watu waliokamatwa na bunduki hizo kuwa ni George Seleman (38), John Maduka (32), wakazi wa Bukombe, Gerald Nhihio (34) na Longino Bernard (33) wakazi wa nchi jirani ya Burundi.
Kamanda Nyakoro aliwataja wengine waliokamatwa na bunduki aina ya FN na mabomu mawili kuwa ni Petro Edward (29), John Maduka (32) Longino Bernard na Masumbuko Betri (33) na kuwa tayari wamefikishwa mahakamani.
Aliongeza kuwa, katika operesheni hiyo, jeshi hilo lilifanikiwa kuokota bunduki moja aina ya SMG na risasi 66 ikiwa imefukiwa katika makaburi ya Nyihogo wilayani Kahama.
Kadhalika, alisema katika msako huo, jumla ya magobore 22 yalikamatwa na watuhumiwa 21 waliokuwa wanayatumia kwa shughuli zinazodhaniwa kuwa ni za kijambazi.
Aidha, alisema magobore mengine matatu yalisalimishwa katika kituo kidogo cha polisi cha Lunzewe wilayani Bukombe.
Wakati huo huo, watu sita wanashikiliwa kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.
Kamanda Sirro aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Rojas kazungu (38), Marubu Sosoma (34), Muhare Matiku (37) na Yusuf Juma (42). Wengine ni Suzana Daud (50) na Kashija John (38).
Alisema watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
|