03 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

`Pelekeni maombi yenu CRDB, NMB`
 
2007-01-03 08:57:48
Na Joseph Mwendapole

Serikali imewataka wananchi wote walioandika michanganuo ya kuomba fedha za mkopo zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, kuanza kupeleka maombi yao kwenye benki za CRDB na NMB.

Rais Kikwete alitoa Shilingi bilioni moja kwa kila mkoa kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na wakati ili kukuza mitaji yao.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kapteni (mstaafu), John Chiligati, wakati wa mahojiano na Nipashe ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Waziri Chiligati alisema wale wote ambao wameandika michanganuo ya miradi na kupitishwa kwenye kamati za Vijiji, Kata na Wilaya wanaweza kuomba na kupewa fedha hizo kuanzia sasa.

Alisema serikali ilishatoa Sh. bilioni 10.5 kwa benki hizo tangu Novemba, mwaka jana, ili zitumike kama dhamana ya kuwakopesha wafanyabiashara hao wadogo na wakati.

“Tulishawapa Sh. bilioni 10.5 ambazo zitatumika kama dhamana ya kuwakopesha wananchi na benki hizo zitakopesha mara tatu ya fedha ambazo serikali imewapa, ” alisema.

Aidha, alisema tayari serikali imeshatoa mafunzo kwa watu 2,000 ambao watatumika kufundisha wafanyabiashara hao namna ya kupata mikopo hiyo na kuitumia.

Alisema waliopata mafunzo hayo ni maofisa ushirika, maofisa maendeleo ya jamii, mipango na wanaoshughulikia mikopo kwenye benki za CRDB na NMB.

Alisema maofisa hao wameanza kwenda vijijini kutoa mafunzo katika ngazi za vijiji, kata na wilaya ili kuwawezesha walengwa kujua namna ya kupata fedha hizo.

Alisema walichukua maofisa watatu kutoka kila halmashauri na kwamba mafunzo hayo yaligawanywa katika kanda tano ambazo ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Dodoma.

“Serikali ilitaka kwanza kuhakikisha hawa walengwa wanapata mafunzo wajue utaratibu huu unavyokuwa na namna ya kukopa maana wengi hawajawahi kukopa, ” alisema Waziri Chiligati.

Alisema mikopo hiyo itatolewa kwa watu binafsi, vikundi na vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) na kwamba kiasi cha kukopa kitategemea mradi ulioombewa fedha.

Waziri Chiligati alisema serikali itahakikisha kamati zilizowekwa kusimamia utaratibu huo zinafanya kazi kwa ufanisi, ili walengwa pekee ndio wapate mikopo hiyo.

“Fedha hizi ni kwa ajili ya watu maskini lakini wajanja hawakosekani, sasa sisi tutasimamia kuhakikisha walengwa tu ndio wanapata, ” alisema.

Aidha, Waziri Chiligati aliwataka wahusika kutoogopa kukopa fedha hizo na kwamba bado kuna watu wanaoona aibu kuwa na madeni.

Alisema watu wengi walioendelea na kufanya biashara kubwa wamekopa na hatimaye kulipa madeni yao.

Mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alitoa Sh bilioni 21 ambazo zitamika kukopesha wafanyabiashara wadogo nchini ili kupamabana na umasikini.

Zilizosambazwa mikoani ili kukopeshwa ni Sh bilioni 10.5 na Sh bilioni 10.5 zilizosalia zitabakia katika mabenki kama dhamana ya mikopo hiyo.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.