|
MOAT yasikitishwa na kauli ya Waziri
2007-01-03 08:58:57
Na Mwandishi wetu
Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT), kimesema kimesikitishwa na kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Muhammed Seif Khatib kwamba wamiliki wake wanavitumia vyombo hivyo vibaya kupotosha wananchi.
Hayo yamo kwenye tamko la chama hicho lililotolewa jana, Jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Katibu Mtendaji wake, Bw. Henry Muhanika.
Tamko la MOAT, linafuatia kauli ya Waziri Khatib iliyodai kuwa, wamiliki wa vyombo vya habari wanapinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari.
Alitoa kauli hiyo alipokutana na waandishi wa habari mjini Dodoma mwezi uliopita, kuzungumzia suala la muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari.
Muswada huo unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni Aprili, mwaka huu.
“Baada ya mazungumzo na waandishi wa habari, Waziri alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akisema kuwa, wamiliki wa vyombo vya habari nchini pekee wamejipa haki wasiyoistahili ya kuukataa muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari,” tamko lilisisitiza.
Aidha, lilisema Waziri alikaririwa pia akisema wadau wa sekta ya habari sio wamiliki wa vyombo vya habari pekee na kuongeza kuwa Wamiliki wa vyombo vya habari wanayo haki ya kutoa mawazo yao ya kuuboresha na sio kuukataa muswada husika kwa vile wanaoweza kuukataa ni wabunge tu, ambao ni wawakilishi wa wananchi.
“Wamiliki wa vyombo vya habari wamesikitishwa na hali hii kwa vile wanaamini kwamba, Waziri wa Habari, Utamadumi na Michezo ambaye pia anamiliki chombo cha habari, anajua kwamba wamiliki wa vyombo vya habari hawajafanya mkutano wowote au kuweka mkakati wa kuwapotosha wananchi juu ya suala hili.
Aidha, tamko lilisema, wamiliki wa vyombo vya habari wanahisi kwamba kauli hiyo inalenga kuwagawa wadau katika suala la kujadili muswada wa kurekebisha sheria ya vyombo vya habari.
“Ni matumaini ya Wamiliki wa vyombo vya habari kuwa wananchi kwa ujumla na waheshimiwa wabunge, wataelewa ukweli kuhusu suala hili,” lilisema sehemu ya tamko hilo.
Hata hivyo, chama hicho kimesema kinakubaliana na Waziri kwamba, wamiliki wa vyombo vya habari sio wadau pekee katika sekta ya habari.
“Jambo hili ni wazi vinginevyo neno wadau linapoteza maana yake,” tamko hilo lilifafanua.
Lilisema pia ni matumaini ya wamiliki wa vyombo vya habari kwamba, Waziri atayatafakari aliyoyasema kuhusu wamiliki wa vyombo vya habari na kuonyesha uungwana kwa kuomba msamaha pale alipokosea.
MOAT imesema wamiliki wa vyombo vya habari wameshangazwa na kauli ya Waziri kwamba wao pekee wamejichukulia haki ya kuukataa muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari.
“Wamiliki wa vyombo vya habari wanawatangazia wananchi kwamba, hawajafanya kikao chochote peke yao na kutoa tamko kwa maneno au kwa maandishi kwamba wanaukataa muswada wa marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari,” tamko la MOAT liliongeza.
Liliongeza “ukweli ni kwamba, wamiliki wa vyombo vya habari wameshiriki katika mikutano miwili ya wadau wa vyombo vya habari iliyofanyika Dar es Salaam mwezi uliopita, mmoja katika Hoteli ya Sea Cliff na mkutano mkuu wa Baraza la vyombo vya habari Tanzania uliofanyika Kurasini ambapo suala la muswada wa kurekebisha sheria ya vyombo vya habari lilijadiliwa.”
Lilisema katika mikutano yote miwili, wawakilishi wa MOAT walikubaliana na wadau wengine kwamba, muswada kama ulivyo haukubaliki kwa wadau na wengine na kwa sababu hiyo wadau wapewe fursa ya kutoa mapendekezo mapya kabla Serikali haijasonga mbele kuchukua hatua zaidi juu ya muswada huu usiokubalika.
“Msimamo huu haukuwa wa MOAT, bali ulikuwa ni msimamo wa wadau wote walioshiriki katika mikutano hiyo.” MOAT imesisitiza.
Tamko hilo lilisema wamiliki wa vyombo vya habari wanasisitiza kwamba, mikutano hiyo haikuwa ya MOAT.
“Katika mchango wake kwenye mikutano hiyo ya wadau, MOAT ilisisitiza kuwa, kwa vile muswada wa marekebisho ya sheria husika unavipunguzia vyombo vya habari uhuru wa kupata habari muhimu za Serikali, kitendo hiki hakilingani na matamshi ya Serikali ya Awamu ya Nne ya kuwa na utawala bora, uwazi na kupiga vita rushwa katika jamii,” tamko lilisema.
Aidha, Wamiliki wa vyombo vya habari wanahisi kwamba, kauli hiyo inalenga kuwagawa wadau katika suala la kujadili muswada wa kurekebisha sheria ya vyombo vya habari.
|