03 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Mawakili wa Dito watishia kwenda Mahakama Kuu
 
2007-01-03 09:00:33
Na Rosemary Mirondo

Mawakili wanaomtetea aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kapteni Ukiwaona Ditopile anayetuhumiwa kwa mauaji, wametishia kwenda Mahakama Kuu kulalamikia ucheleweshaji wa kesi hiyo.

Mawakili hao ni Dk. Ringo Tenga anayesaidiwa na Profesa Jwan Mwaikusa na Bw. Cuthbert Tenga, walitoa tishio hilo jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Bw.Sivangiliwa Mwangesi.

Walitoa tishio hilo baada ya upande wa mashtaka uliokuwa unaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kenyella, kudai kuwa jalada halisi la kesi hiyo lipo kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kusoma ushahidi na vielelezo vilivyokusanywa.

Bw. Kenyella alidai kuwa, baada ya mkuu huyo kuridhika na ushahidi uliokusanywa, atalipeleka jalada hilo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa hatua zaidi.

Aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa madai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga ombi hilo, kwa madai kuwa hoja hiyo haijawaridhisha kwa vile sababu hizo ni taratibu za kiutawala na kusisitiza kuwa jalada la kesi hiyo, bado lipo mikononi mwa polisi.

“Sioni kama kuna hatua yeyote, naona kama Upande wa Jamhuri unatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa wakati mteja wetu bado anasota rumande na jalada lina randa randa polisi,” alisema wakili Tenga.

Bw. Tenga alidai kuwa ni karibu miezi mitatu sasa, jalada bado linarandaranda polisi.

Aliongeza kuwa endapo Upande wa Jamhuri utashindwa kukamilisha upelelezi wao watakwenda Mahakama Kuu kufuatilia Katiba ili mteja wake aweze kupata haki.

Hata hivyo, Bw.Kenyella alidai kuwa upande wa mashtaka haujavunja Katiba kwasababu kesi kubwa hususan za mauaji huchukua muda mrefu.

Aliongeza kuwa upande wa utetezi umeiomba mahakama hiyo kwenda Mahakama Kuu kutoa malalamiko yao wakati Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Hakimu Mwangesi aliutaka upande wa mashtaka, kukamilisha upelelezi wa shauri hilo ili Januari 15, mwaka huu itakapotajwa, watoe jibu la kueleweka.

Awali, upande wa utetezi kupitia wakili wake Bw. Nimrod Mkono, pia uliwahi kulalamika kuwa upande wa mashtaka, unachelewesha kesi kwa kufanya uzembe na kuongeza kuwa kesi hiyo ipo mahakamani hapo kwa mpito kwa kuwa inasubiri kwenda Mahakama Kuu.

Katika kesi hiyo, Ditopilie anadaiwa kuwa, Novemba 4, mwaka jana, saa 1:00 usiku, katika barabara ya Bagamoyo na Kawe, jijini Dar es Salaam, alimuua dereva wa daladala Hassan Mbonde, kwa kumpiga risasi.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 15, mwaka huu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.