04 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Kupima afya ni kinga ya awali kutambua hali ya afya
 
2007-01-04 10:10:44
Na Badru Kimwaga

Kwa namna yoyote ile, upimaji virusi ni kinga ya awali kabisa ya mtu kujitambua hali yake ya kiafya na kumpa uhakika wa kupanga mipango yake kuhusu maisha yake ya baadaye.

Ugonjwa wa Ukimwi ambao ulijitokeza sana kuanzia miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1970 hivi, umekuwa chanzo kikubwa cha vifo vya watu wengi walioambukizwa ugonjwa huo.

Eneo la kusini mwa jangwa la Sahara ni miongoni mwa maeneo ambayo yameathiriwa sana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo hadi sasa hauna kinga wala chanjo, licha ya utafiti mwingi unaoendelea katika nchi mbalimbali karibu duniani kote na wataalamu mabingwa wa tiba ya magonjwa ya binadamu.

Dawa ambazo zimepatikana hadi sasa zinazoendelea kutumiwa ni zile ambazo zinapunguza makali ya ugonjwa huo, kudhibiti magonjwa nyemelezi na kurefusha maisha ya muathirika.

Katika hali hiyo, kabla ya mtu kupima afya yake, hupatiwa ushauri nasaha kwa ajili ya kumtayarisha kupokea matokeo yoyote yale yatakayopatikana kwenye kipimo chake kama ameathirika na VVU au la.

Ushauri nasaha ni muhimu sana katika kumuandaa muhusika ili asikate tamaa, kutimiza misingi ya afya bora kama vile kuacha kuvuta sigara, tumbaku na matumizi ya dawa za kulevya ambazo huzidi kuathiri afya yake na kumsababisha matatizo mengi zaidi ya kiafya.

Kama hiyo haitoshi, mtu aliyeambukizwa virusi vya Ukimwi ni binadamu mwenye hisia zote za kibinadamu, kwa hiyo kupimwa kwa afya yake kutasaidia kupatiwa ushauri wa kuacha kufanya tendo la ndoa kwa sababu kuendelea kufanya hivyo ni kwamba anaweza kujikuta akiambukizwa tena virusi vya aina nyingine na hivyo kulifanya tatizo lake kuwa kubwa zaidi.

Endapo itashindikana kufuata ushauri huo, ni kwamba mtu huyo anatakiwa afanye huku akitumia kondom ili kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.

Na kwa upande wa wanawake wanatakiwa wajizuie kupata mimba vinginevyo kutaathiri zaidi afya yao ikiwa pamoja na kuhatarisha maisha ya kiumbe kitakachozaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za wataalamu wa afya ni kwamba mtu aliyeathirika ambaye anataka kurefusha maisha yake, anatakiwa ajishughulishe na kazi zake ila kama atakuwa amedhoofu inabidi apumzike vya kutosha na la muhimu zaidi kutibiwa kila anapopata dalili za ugonjwa wowote au vidonda vya wazi.

Ukweli uko bayana kuwa, vijana wengi wenye moyo wa ujasiri wameweza kujadili afya zao na wengine na kueleza matokeo ya vipimo vyao, hali ambayo kwa kiasi kikubwa imewatia moyo vijana wengi hata kuchukua uamuzi wa kijasiri wa kupima afya zao na kukabiliana na matokeo yoyote yale yatakayojitokeza.

Vituo mbalimbali vinavyojishughulisha na utoaji wa ushauri nasaha vinaendelea kuwahamasisha vijana kupima VVU kwa njia mbalimbali zikiwemo warsha, midahalo, semina na sanaa zikiwemo michezo ya kuigiza na ngoma.

Hali hiyo imekuwa ikichangia sana kuibua hamasa miongoni mwa vijana na kujitokeza kupima afya zao.

Kwa mujibu wa takwimu za baadhi ya vituo mbalimbali vinavyoendelea kupokea watu wanaoenda kupima afya zao kwa hiari, idadi ya wasichana wanaojitokeza ni wengi zaidi kuliko wavulana.

Kwa nini watu wanaamua kwenda kupima ili kujua hali zao kiafya?

Kutokana nahali halisi ilivyo ni kwamba vijana au watu wengi wamekuwa hawana uhakika wa afya zao.

Kwa sababu mtu unaweza kujilinda vilivyo ili usitumbukie katika hatari ya maambukizi, lakini ya Mungu mengi huweza kujua mwenzako unayeshirikiana naye katika tendo la ndoa ni mwaminifu kiasi gani.

Sababu nyingine ambayo imekuwa ikiwafanya vijana wengi kupima afya zao ni pale wanapotafuta nafasi za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ambapo hutakiwa kupima afya zao.

Kwa vijana wengine wanakwenda kupima afya zao kwa sababu wanataka kuanzisha mahusiano yao ya kimapenzi ambapo wanataka kuwa na uhakika wa kila mmoja kuwa ana hali gani ili waangalie uwezekano wa kuchukua tahadhari au la.

Wakati mwingine watu wamejikuta wakilazimika kupima afya zao kwa sababu ya kutakiwa kufanya hivyo kama sharti la kuajiriwa kazi.

Hatua nyingine muhimu ambayo imekuwa ikiwasukuma watu kuamua kupima afya zao ni pale wanapofikia uamuzi wa kuchukua maamuzi muhimu ya kufunga ndoa na kuamua kutafuta mtoto.

Kutambua afya za wazazi watarajiwa kabla ya kushika mimba, kuna machango muhimu sana wa kupunguza hatari ya maambukizi kwa mtoto akiwa tumboni,wakati wa kujifungua na mara nyingine wakati wa kunyonyesha.

Kwa namna yoyote ile, ni suala jema kabisa kwa watu wanaotaka kufunga ndoa, kuamua kuvunja ukimya wa wazazi au viongozi wa dini kuwafahamisha vijana wao umuhimu wa kupima afya zao (VVU) kabla ya kufunga ndoa.

Kituo cha upashanaji habari na mafunzo cha Kati kilichopo Buguruni cha shirika lisilo la kiserikali Kiota Womens Health and Development Organisation (KIWOHEDE) kimeweza kushirikiana na Makanisa, Misikiti katika suala la kuifahamisha jamii (waumini) umuhimu wa kupima VVU kwa kufanya mikutano na viongozi wao na wakati mwingine washauri hupewa nafasi siku za ibada ili kuwafikishia waumini ujumbe huo.

Viongozi waliweza kuweka mikakati kwamba watawashawishi vijana katika makanisa/misikiti yao kupima virusi vya Ukimwi kabla ya ndoa.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamekuwa wagumu kukubaliana na ushauri huo kwa kile kinachosemwa kuwa kama vijana wao wakikutwa wameambukizwa itawasababishia kuwapotezea bahati zao za kufunga ndoa na hii itakuwa mzigo kwa wazazi wao.

Kwa namna yoyote ile juhudi za kipekee na za nguvu zinahitajika ili kuwaelimisha wazazi hao ili wafahamu faida na hasara za kukaa kimya na kuhatarisha maisha ya vijana wao mara baada ya kuanza mahusiano bila ya kupima afya zao.

Halikadhalika viongozi wa serikali katika ngazi za mitaa, kata na wilaya wanatakiwa kutoa michango yao muhimu katika kuwaelimisha watu kupima afya zao.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.