04 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Wanaohifadhi majambazi tuwafichue bila kuwaonea aibu
 
2007-01-04 10:11:44
Na Mhariri

Sasa imebainika rasmi kwamba kuna baadhi ya wananchi wilayani Bagamoyo ambao huwaficha majambazi wanaoendesha uhalifu katika jiji la Dar es Salaam.

Inadaiwa kwamba kuna baadhi ya wananchi katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo, ambao wamejenga urafiki na majambazi kwa kuwapa hifadhi mara tu wanapofanya vitendo vya uhalifu Jijini Dar es Salaam.

Tunadiriki kusema kwamba watu wa aina hii ni wabaya na hatari zaidi pengine kuliko hata majambazi wenyewe.

Watu wanaowapa hifadhi majambazi ni wasaliti wakubwa wa juhudi zinazofanywa na serikali katika kupambana na wahalifu nchini.

Kibaya zaidi ni kwamba miongoni mwa watu wanaowapatia hifadhi majambazi ni viongozi wa vijiji, ambao walipaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwafichua na kuwapeleka katika vyombo husika ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Imeelezwa kwamba, majambazi wengi wanaofanya uhalifu katika mkoa wa Dar es Salaam, hukimbilia katika baadhi ya vijiji vya Kata ya Miono, wilayani Bagamoyo.

Diwani wa Kata hiyo, Bw. Issa Msakuzi, anakiri kuwepo kwa majambazi katika vijiji vya kata hiyo.

Diwani huyu anasema Kata hiyo imekuwa ikisumbuliwa na majambazi kwa muda mrefu na kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya kwa sababu majambazi yenyewe hulindwa na watu ambao wengine ni jamaa zao.

Ndiyo maana tunaunga mkono wito wa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Luteni Kanali (Mstaafu) Serenge Mrengo, wa kuvitaka vikosi vya ulinzi na usalama wilayani humo kuwafichua watu wanaowakumbatia majambazi na kuwapatia hifadhi.

Katika kukomesha hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi wampelekee majina ya viongozi wanaodiriki kukiuka maadili kwa kushirikiana na majambazi.

DC Mrengo ameahidi kuyafanyia kazi haraka majina hayo, kutokana na ukweli kwamba watu hao wanapingana na Rais Kikwete katika juhudi zake za kupambana na ujambazi.

Rais tayari ameshaweka bayana kwamba serikali yake imeelekeza nguvu katika kuhakikisha majambazi hayatambi katu.

Kwa kiwango fulani, juhudi hizi zimeanza kuzaa matunda kutokana na kupungua kwa vitendo vya uhalifu ambavyo vilitikisa nusu ya kwanza ya mwaka jana.

Tunapenda kuungana na Luteni Kanali (Mstaafu) Mrengo katika mkakati wake huo, ambao tunaamini utasaidia sana kukomesha vitendo vya ujambazi, hususan katika Jiji la Dar es Salaam.

Ni wajibu kwa wananchi wa maeneo hayo sasa kumpelekea DC wao majina ya watu hao wanaotoa hiafadhi kwa majambazi ili ayafanyie kazi kama alivyoahidi.

Ni matarajio yetu kwamba baada ya kupata majina hayo, atafanya kama alivyoahidi na kwamba hatamuonea haya mtu yeyote, hata kama ni watu maarufu katika maeneo hayo.

Kazi ya kupambana na ujambazi haiwezi kufanikiwa kama wananchi hawatashiriki kikamilifu katika kuwafichua wahalifu kwani wamo miongoni mwao na wanafahamika. Tuwafichue majambazi ili tudumishe amani, utulivu na usalama ndani ya jamii yetu.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.