04 Jan 2007 MAIN PAGE SITE INDEX CONTACT US HELP
  Swahilinews
NAVIGATION
SEARCH
 
SPECIAL  
ARCHIVES  
Print this article Send this article

Daraja lakatika Lugoba
 
2007-01-04 10:24:35
Na Thobias Mwanakatwe, PST Chalinze na Erick Lema

Zaidi ya abiria 3,000 waliokuwa wakisafiri kutoka mikoa ya Kaskazini kwenda Dar es Salaam na kutoka Dar es Salaam, Morogoro na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwenda mikoa ya Kaskazini, wamekwama.

Abiria hao wameshindwa kuendelea na safari zao, baada ya daraja la muda la mto Mkombezi lililopo kijiji cha Lugoba, Wilaya ya Bagamoyo kuzolewa na maji.

Kuzolewa na maji kwa daraja hilo, kulisababisha magari zaidi ya 100 yakiwemo ya mabasi ya abiria na malori yaliyobeba shehena mbalimbali za mizigo, kushindwa kupita.

Daraja hilo la muda, lilijengwa ili kupisha ujenzi wa daraja jipya linalojengwa na mkandarasi wa kampuini ya M/S Southern Link Ltd.

Maji katika daraja hilo yalianza kufurika kuanzia jana saa 2:00 asubuhi.

Baadhi ya wenyeji wa eneo hilo, walisema daraja hilo lilifurika maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali wilayani Bagamoyo.

Walisema mvua hizo zimesababisha maji kujikusanya kutoka mto Mkombezi na mto Rusako kutoka katika Milima Uluruguru, mkoani Morogoro.

PST iliyashuhudia baadhi ya mabasi yaliyoshindwa kuendelea na safari zake kuwa ni ya kampuni ya Dar Express T 273AHV na T308 AFU.

Mengine ni T213ACK mali ya kampuni ya Saloom, T849 ALC ya kampuni ya Tahweed, T408 AMJ, mali ya kampuni ya Osaka na E638 la kampuni ya Serengeti.

Kutokana na daraja hilo kuzolewa na maji, polisi waliamua kuyazuia magari yote kupita eneo hilo.

Meneja wa Wakala wa Serikali wa Barabara na Mizani (TANROADS) mkoani Pwani, Bi. Happiness Mgalula aliyefika eneo la tukio muda mfupi baadaye, aliagiza kupelekwa kwa mashine ya kunyonya maji ili kuwezesha magari madogo kupita katika daraja jipya.

Hata hivyo, Bi. Mgalula alisema magari makubwa hayataruhusiwa kupita katika daraja hilo jipya ambalo ujenzi wake haujakamilika.

Kutokana na hali hiyo, baaadhi ya abiria kuhamishiwa kwenye mabasi mengine yaliyokuwa upande wa pili ili waendelee na safari.

Hata hivyo, zoezi hilo lilifanyika kwa mabasi yanayomilikiwa na kampuni moja huku abiria waliokuwa katika kampuni isiyokuwa na mabasi mengine, wakiendelea kusota eneo hilo bila kujali hatma yao.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Dk. Christine Ishengoma, aliwasili eneo la tukio baadaye sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Luteni Kanali (mstaafu), Serenge Mrengo.

Akiwa eneo hilo, Luteni Kanali Mrengo aliwataka abiria waliokwama, kusaidia kuweka kifusi kwa kutumia majembe ya mikono ili magari yao yaweze kupita na kuendelea na safari yake.

Hali kadhalika, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Magreth Sitta pamoja na Naibu wake, Bi. Mwantumu Mahiza, walishuhudia tukio hilo wakiwa katika safari zao za kikazi.

Aidha, eneo hilo ghafla lilibadilika na kuwa la biashara hasa za chakula ambapo pia kilikuwa kikiuzwa kwa bei ya kuruka kutokana na mahitaji ya abiria wengi.

Mashine ya kusaidia kupunguza maji katika daraja hiyo iliwasili eneo la tukio saa 8:30 alasiri na kulikuwa na dalili kwamba, magari makubwa yakiwemo mabasi yaliyokwama, yangeanza kuruhusiwa kupita hapo muda wa jioni.

Baadhi ya magari yalilazimika kupitia Bagamoyo na kwenda mikoa ya Kaskazini ama yale yaliyotoka katika mikoa ya huko kuja jijini Dar es Salaam.

Hata, taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa, magari yote yaliruhisiwa kupita katika daraja hilo na kuendelea na safari saa 10:20 jioni.

  • SOURCE: Nipashe
Habari za Leo
-----------------------------------------------
Maoni ya Mhariri
-----------------------------------------------
Business bits
-----------------------------------------------
Makala
 
Privacy Statement Terms Of Use ©1998-2005 IPPMedia Ltd.  All Rights Reserved.