|
Je, Watanzania tunayathamini maisha yetu?
2007-04-20 08:50:08
Na Michael Kitulizo
Neno bima limekua sio geni miongoni mwa watanzania walio wengi. Bima ya magari, bima ya afya, bima ya moto na kadhalika ni baadhi ya maneno ambayo tumekua tukiyasikia.
Kwa Watanzania walio wengi, neno hili bado limebaki kuwa msamiati isipokuwa kwa baadhi ambao wanaelewa umuhimu wake.
Neno bima maana yake ni mfumo maalumu wa kulinda mali, biashara au watu dhidi ya athari mbalimbali ambapo kundi/kampuni maalum, kwa kulipwa kiasi fulani cha fedha (premium) linachukua majukumu ya kubeba mzigo wa hasara ambayo yaweza kutokea kutokana na athari mbalimbali.
Kwa maana hiyo, kama mtu ataamua kujiwekea bima, aidha ya gari, moto na bima nyingine , atalazimika kuchangia kiasi fulani cha fedha kuendana na makubaliano na kampuni husika, na endapo hasara yoyote itatokea, yenye thamani aidha pungufu, zaidi au sawasawa na kiasi ambacho kimeshachangiwa; kampuni ya bima italazimika kulipa kiasi cha hasara husika kuendana na makubaliano.
Kwa kujiwekea bima, muhusika anadhihirisha ni kwa jinsi gani anavyothamini mali zake. Swali la muhimu kujiuliza leo hii ni je, Watanzania tunajali na kuyathamini maisha yetu?
Je, watanzania tuna tabia ya kuweka bima za maisha yetu au tunajali zaidi mali zetu.
Takwimu zinaonesha kwamba, ni watu pungufu ya laki moja tu (100,000) ndio wana bima ya maisha ikilinganishwa na idadi ya Watanzania iliyo zaidi ya millioni 35. Sababu za idadi hii ndogo zaweza kuwa nyingi, lakini uelewa wa faida zake na gharama zake zaweza kuwa moja ya sababu kuu zinazosababisha idadi hii ndogo.
Kwa kuliona hilo, na kuelewa umuhimu wa bima ya maisha kwa Watanzania, Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT) ilichukua jukumu la kubuni njia muafaka/mbadala itakayowawezesha Watanzania kupata si tu bima ya maisha bali pia bima ya ajali na bima ya kilema cha kudumu, gharama za mazishi na hapo hapo akinufaika na faida za uwekezaji katika dhamana mbalimbali za kifedha.
Njia hii mbadala ni Mfuko wa WEKEZA MAISHA unaojulikana kwa jina la kitaalam kama ULIP – Unit Linked Insurance Plan. Mfuko huu ni muungano wa uwekezaji na faida za bima na unawapa nafasi watanzania wa kipato cha chini, kati au juu kushiriki.
Kama ilivyokuwa kwa Mfuko wa Umoja, mwekezaji katika Mfuko wa Wekeza Maisha atatakiwa kununa vipande ambavyo vitakuwa na thamani ya awali ya Shilingi 100/= kwa kila kipande.
Tofauti na Mfuko wa Umoja, katika Mfuko wa Wekeza Maisha, kiwango cha chini cha kuchangia ni Shilingi Milioni 1 na hakuna kizuizi kwa kiwango cha juu.
Baadhi ya watu wamekuwa wakistushwa na kiwango hicho cha Shilingi Milioni 1.
Kipindi cha uwekezaji katika Mfuko wa Wekeza Maisha ni miaka 10 na hivyo basi tunaposema kuwa kiwango cha chini cha kuchangia na Shilingi milioni 1 ina maana ya kuwa, ndani ya kipindi hicho cha miaka 10, mwekezaji atatakiwa kuwa ameweza kuchangia shilingi milioni 1.
Mwekezaji anaweza kuchangia fedha hiyo aidha kwa mkupuo (mara moja) au kwa vipindi tofauti, yaani kwa kila mwaka, nusu mwaka au kila mwezi kuendana na uwezo na matakwa ya mwekezaji.
Hivyo basi, kwa kiwango cha chini cha shilingi milioni 1, mwekezaji atatakiwa kuchangia aidha, Shilingi 100,000/= kila mwaka, Shilingi 50,000/= kila baada ya miezi sita au Shilingi 8,340/=kwa kila mwezi.
Kwa nafasi hizo tofauti, Mfuko wa Wekeza Maisha utatoa wigo mpana wa kumwezesha kila Mtanzania kunufaika na matunda ya uwekezaji wake.
Sehemu kidogo ya kiasi kitakachochangiwa (chini ya asilimia 1%) kitatumika kuchangia gharama za bima na sehemu inayobakia itawekezwa katika masoko ya kifedha.
Mfuko wa Wekeza Maisha unatoa faida za bima na uwekezaji.
Faida za bima zitakazotolewa ni pamoja na Bima ya maisha, Bima ya Ajali pamoja na Gharama za mazishi. Faida za uwekezaji ni Ongezeko la thamani ya kipande pamoja na Mkono wa pongezi.
Hivyo basi, Dhamana ya Uwekezaji Tanzania inatoa nafasi nyingine ya kipekee kwa Watanzania kunufaika na Mfuko huu.
Ikumbukwe kuwa Mfuko wa Umoja ambao ulikuwa wa kwanza kuanzishwa na Dhamana ya Uwekezaji Tanzania umekuwa na mafanikio ya kuridhisha ndani ya kipindi cha miaka miwili toka kuanzishwa kwake.
Hili lipo wazi kwani thamani ya kipande imeongezeka na faida inayopatikana ni kubwa ikilinganishwa na faida zinazopatikana katika dhamana mbalimbali za kifedha.
Kwa uzoefu uliopatikana katika kusimamia na kufanikisha Mfuko wa Umoja, tunaamini kuwa Mfuko wa Wekeza Maisha utakuwa ni changamoto kwa Watanzani kuona faida zinazopatikana katika Mifuko ya pamoja ya uwekezaji.
Watanzania , tunatakiwa kujijengea zaidi tabia ya kuweka akiba (savings).
Lakini ili akiba hiyo itumike kutoa nafasi muhimu katika kujenga misingi imara ya maendeleo ya taifa letu, lazima iwekezwe kwa namna bora.
Dhamana ya Uwekezaji Tanzania inatoa na itaendelea kuwapatia Watanzania namna bora ya kuwekeza akiba zao ikitoa fursa sawa kwa wote, wenye kipato cha chini na cha juu.
|