|
Tusisubiri majanga yatokee ndipo tukurupuke
2007-04-21 08:38:26
Na Badru Kimwaga
Awali ya yote niwape pole na salamu za rambirambi wale wote waliopoteza ndugu jamaa na marafiki pamoja na waliojeruhiwa katika ajali ya barabani ya wiki hii iliyohusisha basi la Buffalo na lori la mafuta huko mkoani Kilimanjaro.
Mungu awape subira na afueni katika msiba na majonzi mazito yaliyonayo kwa hivi sasa kutokana na tukio hilo la kuhuzunisha na moja ya muendeleo ya majanga ya taifa hili.
Kama Mtanzania nilishtushwa na ajali hiyo iliyopoteza wenzetu zaidi ya 20 kwa mpigo na jinsi serikali kupitia taasisi zake kama Jeshi la Polisi kuzinduka na kuanza kufuatilia kwa karibu kwa kuyakagua mabasi ya abiria ya mikoani.
Kila mmoja wetu amelisikia jeshi hilo kupitia kwa Mkuu wao IGP, Said Mwema akinguruma siku chache baada ya kutokea ajali hiyo ya Kilimanjaro na pia tumeweza kushuhudia baadhi ya vyombo vya habari vikiwaonyesha askari wa Usalama barabarani wakiyakagua mabasi kituo kikuu cha Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kabla hatujakaa sawa tumeripotiwa tena kuwa, karibu mabasi yote ya kampuni ya basi lililopata ajali hiyo, Buffalo kutoweka barabarani tangu ajali hiyo itokee huku baadhi ya `mikweche` mingine ikipotea mitaani kwa hofu ya kunaswa na masako wa jeshi hilo.
Ni kazi nzuri na inayostahili kupongezwa, lakini napata wasiwasi juu ya mtindo huu wa serikali na taasisi zake kusubiri majanga yatokee ndipo ikurupuke na kuanza kufuatilia.
Mtindo huu haujaanza leo ama jana ni wa siku nyingi, tuliona ilipotokea ajali ya MV Bukoba mwaka 1996, serikali ilizinduka na kuzikagua meli zote za abiria katika Ziwa Victoria na mengineyo ili kuepuka ajali nyingine zaidi, safii...!
Hali hiyo ilitokea pia hata katika ajali za mara kwa mara za barabarani zilizokuwa zikiibuka na kutoweka kila mwaka, kiasi cha kubadilishwa ratiba ya safari za mabasi toka jioni na usiku kucha na kutakiwa kuanza asubuhi na mwisho saa 3 usiku.
Pamoja na mabadiliko hayo, bado ajali ziliendelea kutokea, serikali hiyo hiyo ikaibuka na kuleta vifaa vya kudhibiti mwendo (Speed Governor), ambavyo hata hivyo hatujui viliishia wapi licha ya kwamba havikutoa matokeo mazuri kutokana na baadhi ya wenye mabasi kudaiwa walikuwa wakivilegeza ama kutoviweka kabisa.
Orodha ni ndefu ya ukurupukaji huu wa serikali kila linapotokea janga na kuibuka na staili ya kuzuia majanga mengine yasitokee, ambazo hata hivyo huishia kimya kimya ama kuzimwa baada ya siku chache.
Nani hakumbuki mpaka ilipotokea ajali ya kivuko ya kule Kilombero ndipo ikaelezwa kuwa kivuko kilikuwa kichakavu mno, siku zote haikufahamika ama ni kasumba ya kusubiri janga litokee ndipo wataalamu wetu wafanye kazi ya ukaguzi?
Ajali ya Buffalo imetokea ndio imeibua kuwa ni wajibu wa mabasi hayo yakaguliwa ama mengi yao hayana madereva waliopitia Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) na kadha wa kadhaa.
Leo hii wakazi wa Kigamboni wamekuwa katika hali ya mashaka na hofu juu ya usalama wao maisha yao kutokana na ubovu wa vivuko vya Mv Alina na Kigamboni, lakini kauli za kisiasa zinaendelea kutolewa bila kuenyeshwa jitihada za kuwasaidia.
Inasubiriwa vivuko hivyo vilete maafa ndipo wahusika waibuke na kusema vivuko hivyo havikufaa wakati ukaguzi ungepaswa kufanywa sasa na tahadhari zikachukuliwa mapema kabla ya kutokea kitu kama hicho.
Waswahili husema Kinga ni Bora Kuliko Tiba na Jihadhari Kabla ya Hatari, lakini sijui kwa viongozi wetu misemo hii kwao inatafsirika vipi?
Tunajua tahadhari ama kinga nyingine zinahitaji fedha nyingi na serikali pengine kwa majukumu iliyonayo inakuwa vigumu kwake kuweza kutekeleza kila jambo, lakini hata kutambua kuwa mabasi mengi ya mikoani yanahitajika kukaguliwa mara kwa mara kujua ubovu wake na kuhakikisha yanaendeshwa na madareva wenye sifa zinazofaa?!
Jeshi la Polisi idara ya Usalama Barabarani wapo kwa ajili ya kufanya kazi gani?
Kupiga `mabao` daladala za jijini Dar es Salaam ama kuyakamata malori ya mkaa na yale ya mchanga ili kuwatoa upepo?
Kama sio sasa ukaguzi huo unashikaje kasi baada ya kutokea ajali ya Buffalo.
Sina shaka serikali na taasisi zake zitakuwa makini na kuchukua tahadhari mapema bada ya kusubiri ajali ama maafa yatokee ndipo waibuke na kuanza kujipanga upya kupambana na hali hiyo.
Tukumbuke kuwa, siku zote mchelea mwana kulia hulia mwenyewe, tahadhari kabla ya hatari ni muhimu na silaha nzuri ya kuliokoa taifa na majanga yanayoweza kuzuilika kuliko mtindo wa kukurupuka mambo yanapokwepa kombo.
|