|
``Kuliko niache kazi...heri nikuachilie mbali wewe!`
2007-04-22 10:54:59
Na Anti Flora Wingia
Wiki chache zilizopita, katika safu hii tulijadili fumanizi la ofisi, huku nikijaribu kusisitiza kwamba ofisi ni mahali paheshimika na siyo pa kufanyia mambo ya hovyo, kipuuzi kama vile kujistarehesha kimwili na kadhalika. Baadhi ya wasomaji walijaribu kutoa maoni yao mbalimbali kuhusiana na jambo hilo.
Leo, tumsikie msomaji wetu ambaye pamoja na kuunga mkono wale wote wanaopinga uchimvi huo, yeye anadai yaliwahi kumkuta na hapa anatoa ushuhuda wake. Anaanza hivi katika email yake aliyoituma kwa safu hii;-
Hi Aunt Florah,``Mimi ni kijana mwenye umri wa kati, ninayeishi nje ya nchi kwa sasa kimasomo. Nimesoma mada yako hivi karibuni kuhusu fumanizi la ofisini kwa masikitiko makubwa. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba imenitonesha kovu, kwa kidonda nilichopata kwa uchungu mwaka 2002.
Nilikuwa na mchumba wangu aliyekuwa anafanya kazi kwenye kampuni moja ya mwanasheria maarufu hapo jijini Dar. Huyo mpenzi wangu kila kukicha alikuwa akiniambia kuwa anaenda kazini mpaka Jumapili, siku za sikukuu muhimu.
Siku moja nikamuuliza mfanyakazi mwenzie kulikoni mwenzangu afanyishwe kazi mpaka sikukuu? Akanijibu kuwa huyo ana yake, kwani ni mpenzi wa bosi.
Kwa bahati mbaya huyo bosi wake alikuwa ameoa binti mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika moja ya benki maarufu na ya zamani hapo jijini Dar. Nilichunguza na kuhakikisha kweli mpenzi wangu anatembea na bosi wake...!!nikamuomba aache kazi nimtafutie sehemu nyingine.
Akanijibu kuliko aache kazi pale ni kheri aniache mimi.!!!Mungu mkubwa kumbe na yule mke wa bosi alishayajua hayo ya mpenzi wangu na mumewe. Jumapili moja mke wa bosi akaweka mitego yake, akawanasa wakila uroda ofisini kwao.
Yule bosi kwa hasira akampiga yule mama(mkewe) mpaka akalazwa wodi ya wagonjwa mahututi-ICU Muhimbili. Hata hivyo, baada ya siku tatu yule mama alifariki dunia. Mpenzi wangu na bosi wake wote wakawekwa ndani na kufunguliwa kesi ya mauaji..!!!!, Ama kwa hakika mshahara wa dhambi ni mauti......penzi la ofisini limezua mambo.....!!!!!!!!!!,
H.K.B
USA.
Mpenzi msomaji, hivyo ndivyo anamaliza msomaji wetu huyu anayesoma nchini Marekani, na hakika, hayo ndiyo mambo ya fumanizi. Kumbe wakati mwingine yanasababisha vifo?
Kwa ujumla, inaonyesha jinsi watu wasivyo waaminifu ndani ya ndoa zao na wakati huo huo walivyo wakali pale yanapowakuta makubwa kama bosi huyo.
Kwanza, ufirauni ule aliufanya siku ya Bwana-JUMAPILI- inayopaswa kutakaswa kwa gharama zote.
Ni siku ya mapumziko na pia kushiriki Ibada makanisani na hata sala majumbani mwetu. Hata uwapo ofisini ukipata muda pia sali kumuomba Mungu rehema zake na vipaji vyake siyo kufanya madudu machafu.
Sasa jamaa badala ya kwenda kusali yeye anabanjua na kuivunja amri ya sita, tena na kimada chake huku mke akijikunyata.
Na hata mke huyu alipomfumania live ofisini, bado alimuadhibu kwa kipigo badala ya kuomba radhi. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo. Huo ni ukatili wa mwanadamu uliovuka mipaka.
Ukosefu wa uaminifu ndani ya familia, nyumba zetu umesababisha mambo mengi likiwemo hili la fumanizi. Unajua tena mnyama simba anapokuwa katika mawindo yake hataki mtu yoyote aingilie anga zake hizo. Ni yeye na windo lake. Anapotokea mtu au mnyama mwenzake, lazima awe mbogo.
Hicho ndicho kilichotokea kwa bosi yule. Yeye akiwa katika windo lake, ghafla mama watoto akamvamia. Matokeo yake ni kibano kilichopelekea kulazwa mahututi na baadaye kuaga dunia kama alivyodokeza msomaji wetu hapo awali katika makala hii.
Mama watoto alikuwa katika harakati za kupima uaminifu wa mumewe. Na bila shaka ni hofu ya kugawana pato la familia na hawara za mumewe. Isitoshe, kikubwa zaidi na cha msingi pia ni maambukizi ya maradhi hatari kama vile ukimwi unaotokana na zinaa.
Lakini, kwa bahati mbaya wakati anajaribu kulinda mji wake, akajikuta anapoteza maisha. Swali ni je, uamuzi wa bosi yule kumpiga mkewe hadi kumsababishia kifo ulikuwa sahihi? Na je, ipo faida yoyote aliyopata kwa uamuzi ule?
Au mama watoto alifanya kosa kwenda ofisini kufuatilia nyendo za mumewe? Kama unayo maoni kuhusiana na maswali hayo mpenzi msomaji, niminyie kwenye mtandao kupitia email ya safu hii tuelimishane.
Kisa hicho kinanikumbusha ile methali isemayo ‘mtaka yote kwa pupa hukosa yote. Bosi aliendekeza tamaa za kimwili na kusahau utakatifu wa Mungu ndani ya ndoa yake.
Mke anamtaka ndani ya nyumba na wakati huo huo kimada wa nje anamtaka, matokeo yake anakosa wote.
Mke sasa ni marehemu, kwa mujibu wa mtoa habari hizo na mwanaume(bosi) na kidosho wamefunguliwa kesi ya mauaji kwa hiyo wote wako rumande.
Wapo watu wanaojifanya wajanja na kwamba hawawezi kugundulika katika ujanja wao. Hawa husahau kuwa ndege mjanja siku zote hunaswa kwenye tundu bovu.
Isitoshe wengine husahahu kuwa siku za mwizi ni arobaini. Utafanya mambo yako ya kifedhuli kila wakati bila kubambwa. Lakini usijidanganye kwamba huwezi kunaswa hata siku moja.
Kumbuka siku ya kufa nyani, miti yote huteleza. Au siyo? We shauri yako. Tumuombe sana Mwenyezi Mungu azijenge upya nyumba/familia zetu. Nyingi zimeingiliwa na ibilisi na hivyo maisha kutikisika...kisa kutoweka kwa uaminifu.
Wasalaam
Email: fwingia@yahoo.com
|